1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WWF kuzuia uchimbaji wa mafuta Virunga

1 Agosti 2013

Shirika la kimataifa la kuhifadhi wanyama na mazingira, WWF, limezindua ripoti juu ya umuhimu wa kuilinda mbuga ya wanyama ya Virunga iliyopo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Milima ya Virunga
Milima ya VirungaPicha: picture-alliance/united-archives/mcphoto

Ripoti ya WWF iliyopewa jina la "Thamani ya kiuchumi ya Mbuga ya Virunga" imeeleza kwamba mbuga hiyo inaweza kuipatia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zaidi ya dola za kimarekani bilioni 1 kwa mwaka iwapo itatumika kwa njia endelevu.

Mbuga ya wanyama Virunga ilizinduliwa mwaka 1925 na hivyo kuifanya mbuga ya zamani kuliko zote barani Afrika. Inahifadhi zaidi ya aina 3,000 za wanyama, wakiwemo sokwe wa milimani walioko hatarini kutoweka. Mwaka 1979, mbuga ya Virunga iliorodheshwa kuwa eneo la turathi la shirika la Umoja wa Mataifa la sayansi na utamaduni UNESCO.

Uchimbaji wa mafuta au ulinzi wa mazingira?

Kwa sababu hiyo, mashirika ya kulinda mazingira, likiwemo shirika la WWF, yanaupinga uamuzi wa serikali ya Kongo wa kuyakaribisha makampuni ya nje kuja kuchimba mafuta katika eneo la mbuga hiyo.

Sokwe mbugani VirungaPicha: Reisedoktor/Wikipedia

Raymond Lumbuenamo, ambaye ni mkurugenzi wa WWF nchini Kongo anatoa ujumbe huu kwa serikali: "Mmesaini makubaliano ya kimataifa yanayokataza uchimbaji wa mafuta au nishati nyingine kufanyika mbugani. Hivyo naomba mheshimu sheria mlizojiwekea wenyewe." Mwezi uliopita, UNESCO iliyataka makampuni ya mafuta ya Total na SOCO International, kubatilisha vibali walivyokuwa wamepewa na serikali ya Kongo kwa ajili ya kuchimba mafuta mbugani. Kampuni ya Total ilikubali kuheshimu mipaka ya mbuga ya Virunga. Hivi sasa, SOCO International ndiyo kampuni pekee yenye mpango wa kuchimba mafuta katika eneo la hifadhi ya kitaifa.

Serikali inataka maslahi ya mafuta

Raia wa Kongo nao wanapinga uchimbaji wa mafuta mbugani. "Pamekuwa na maandamano ya kuilinda mbuga ya Virunga. Wakati mwingine wanajeshi waliingilia kati na kukataa maandamano. Lakini bado watu wanasema ndiyo, tunaitaka mbuga hii," anaeleza Lumbuenamo wa WWF.

Kampuni ya Total haitachimba mafuta VirungaPicha: picture-alliance/dpa

Shirika la WWF limezindua kampeni inayolenga kuilinda mbuga ya Virunga dhidi ya uchimbaji mafuta. WWF inataka kuiwekea shinikizo kampuni ya SOCO International ili iachane na mpango wake wa kuchimba mafuta huko Virunga au katika eneo lingine lolote la turathi ya UNESCO.

"Tukifuata njia ya uhifadhi itakuwa ya kudumu, tukifuata njia ya mafuta, litakuwa jambo la wakati mmoja tu," anasema Lumbuenamo. Hofu yake ni kwamba serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo itaweka mbele tamaa ya kupata maslahi ya haraka kutokana na mauzo ya mafuta na kusahau kabisa jukumu lake la kuhifadhi mbuga ya Virunga, iliyo ya kipekee barani Afrika.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/WWF

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi