1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Xi aapa kupambana na ufisadi

17 Machi 2013

Kiongozi mpya wa China, Xi Jinping, ameahidi kuongoza serikali safi na yenye ufanisi zaidi na kupambana na ufisadi baada ya ubadilishanaji wa madaraka kwenye taifa hilo la kikomunisti lenye nguvu kubwa kiuchumi duniani.

BEIJING, Jan. 17, 2012 (Xinhua) -- Chinese Vice President Xi Jinping, also a member of the Standing Committee of the Political Bureau of the Communist Party of China (CPC) Central Committee, secretary of the Secretariat of the CPC Central Committee and vice Chairman of the Central Military Commission, extends his greetings and respect to retired officials at a reception held at the Great Hall of the People in Beijing, capital of China, Jan. 17, 2012. (Xinhua/Li Xueren) (lmm) XINHUA /LANDOV
Xi JinpingPicha: picture alliance/landov

Katika hotuba yake ya mwanzo baada ya kuchaguliwa, Xi amesema kwamba atapigania "kuiinua upya hadhi ya taifa la China," na kutaka kuchukuliwa kwa jitihada za makusudi na kubwa kabisa kuendeleza dhamira ya China kuwa taifa kubwa kabisa duniani.

Uongozi mpya wa China, ambao unatarajiwa kuwa madarakani kwa kipindi cha muongo mmoja kama ule uliotangulia, umesema kwamba utatilia mkazo kwenye matumizi ya kijamii na hatua nyengine za kusambaza maendeleo kwa upana zaidi kwa lengo la kupunguza pengo kati ya matajiri wachache na masikini walio wengi nchini humo, na vile vile kupambana na ufisadi.

Nguvu za kijeshi

Wito huo wa kuipandisha hadhi ya China duniani umekuwa kauli ya kawaida tangu Xi kuchukua nafasi za juu nchini China, ikiwemo ya ukuu wa Chama cha Kikomunisti, uongozi wa jeshi na hii ya uongozi wa dola.

Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi.Picha: AP

Ingawa hajaelezea undani wa namna China itakavyojiimarisha kilimwengu, Xi ana mafungamano makubwa na jeshi la nchi hiyo na amekuwa akilihimiza jeshi lijiimarishe ili "lishinde vita."

China iko kwenye mgogoro wa siku nyingi na Japan juu ya visiwa kwenye Bahari ya Mashariki ya China na pia inalumbana na mataifa mengine jirani juu ya udhibiti wa Bahari ya Kusini ya China.

Hotuba ya Xi ilizungumzia pia ufisadi, ambao aliuita kuwa ni kitisho kwa Chama cha Kikomunisti na kuwataka wajumbe kupingana na tamaa na maisha ya kifahari na badala yake wapambane na tabia ya ufisadi.

Bunge laidhinisha baraza jipya la mawaziri

Kabla ya kukamilisha kikao chake siku ya Jumapili (17.03) , bunge hilo liliidhinisha uongozi mpya wa watu wanaoonekana kuwa wasomi, wengi wao wakiwa na uzoefu mkubwa kwenye siasa za kimataifa, ambao wanaunda baraza la mawaziri lililopewa jukumu la kuuinua uchumi unaozorota na kuijengea China hadhi kubwa ulimwenguni.

Waziri Mkuu mpya wa China, Li Keqiang.Picha: Reuters

Miongoni mwa mawaziri muhimu kwenye baraza hilo jipya ni wale wa fedha, biashara na mambo ya kigeni, ambapo balozi wa zamani nchini Japan, Wang Yi, ametangazwa kuwa waziri mpya wa mambo ya kigeni.

Mawaziri wengine wapya ni pamoja na Lou Jiwei, ambaye anakuwa waziri fedha, akitokea kwenye uongozi wa taasisi maalum uwekezaji kwa mashirika ya umma.

Waziri Mkuu aigeukia Marekani

Katika kile kinachoonekana kama hatua za mwanzo kukabiliana na mataifa ya nje, Waziri Mkuu mpya Li Keqiang, amekanusha vikali tuhuma za Marekani kwamba China inashiriki kwenye udokozi wa mitandao ya Marekani, akisema kwamba serikali yake haiungi mkono ujasusi kwenye mitandao.

Kauli ya Li imekuja baada ya Rais Barack Obama wa Marekani kuingilia kati kulizungumzia suala hilo, ambalo kwa siku kadhaa limekuwa likizungumzwa na maafisa wa ngazi za juu wa Marekani.

"China yenyewe ni muathirika wa mashambulizi ya mitandaoni," alisema Li baada ya mkutano wa bunge. "Nadhani hatupaswi kutoa tuhuma zisizo na msingi wowote dhidi ya wengine na badala yake tunapaswa kujitahidi kufanya yale yatakayochangia kwenye usalama wa mitandao."

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW