Xi amuapisha kiongozi mpya Hong Kong
1 Julai 2017Hayo ameyasema katika hotuba yake yenye maneno makali kuadhimisha miaka 20 ya koloni hilo la zamani la Uingereza kurejea kwa China. Usalaama uliimarishwa katika eneo la bandari ambayo miongo miwili iliyopita , gavana wa zamani wa kikoloni , Chris Patten , akimiminikwa na machozi aliikabidhi Hong Kong kwa China katika sherehe ambayo ilifanyika huku mvua kubwa ikinyesha.
"Jaribio lolote la kuhatarisha uhuru na mipaka ya China pamoja na usalama wake, ni sawa na kupambana na dola ya serikali kuu ya China na mamlaka ya sheria mama ya HKSAR ama kuitumia Hong Kong kuingilia na kuvuruga shughuli dhidi ya China bara katika hatua ambayo inavuka mstari mwekundu na haitakubalika kabisa," amesema Xi.
Chini ya katiba ndogo ya Hong Kong , sheria ya msingi, jimbo hilo ambalo ni sehemu muhimu ya kiuchumi inahakikishiwa uhuru wake kwa "takriban miaka 50" baada ya mwaka 1997. HKSAR ina maana ya jimbo maalum la utawala la Hong Kong, ambalo linaongozwa chini ya utaratibu wa "nchi moja , mifumo miwili" unaoruhusu mamlaka makubwa ya ndani.
Maneno ya Xi ni makali kuwahi kutolewa kwa eneo hilo la kituo cha masuala ya fedha duniani na yanakuja katika wakati wa wasi wasi mkubwa wa kijamii na kisiasa na yanajumuisha kile ambacho wengi katika jimbo hilo la Hong Kong wanaona ni hali inayoongezeka ya kuingiliwa na serikali kuu ya China katika masuala ya ndani ya mji huo.
Alikuwa akihutubia ukumbi uliojaa wageni waalikwa pamoja na watu mashuhuri wengi wao wakiwa ni waungaji mkono serikali kuu mjini Beijing , akizungumza kwa zaidi ya dakika 30 , baada ya kumuapisha kiongozi wa kwanza mwanamke wa Hong Kong, Carrie Lam.
Ghasia za hapa na pale
Vurugu za hapa na pale zilitokea nje ya ukumbi huo wakati wanaharakati wanaodai demokrasia zaidi , baadhi wakiwa na mabango yenye maneno "demokrasia. Utawala wa ndani," na makundi yanayopendelea China walitupiana maneno, huku mamia ya polisi wakiwekwa katika siku hii ya kihistoria ya maandamano mjini Hong Kong.
Waandamanaji kadhaa wanaodai demokrasi walichukuliwa na polisi , wakati makundi kadhaa yanayounga mkono serikali ya China , yakishangilia kwa nguvu na wakipunga bendera kama vile kwa kuonesha ushindi.
Rais Xi Jinping alisema Hong Kong ni huru zaidi kuliko ilivyokuwa hapo kabla lakini akaonya dhidi ya kile alichosema "changamoto ambazo zisizoruhusika" dhidi ya mamlaka ya Beijing.
Lam alichaguliwa na kamati inayounga mkono China , kama walivyo watangulizi wake, na tayari anaonekana na wakosoaji kuwa ni kibaraka wa China katika mji ambako wengi wamekasirishwa na China inavyoongeza mbinyo dhidi ya uhuru wa watu karibu milioni nane.
Lam alikula kiapo kuingia madarakani chini ya bendera ya taifa la China katika kituo cha makutano katika bandari mjini Hong Kong, kabla ya kushikana mikono na Xi.
Kuapishwa kwake kunakuja siku moja baada ya wizara ya mambo ya kigeni ya Beijing kutangaza kwamba waraka uliotiwa saini na Uingereza na China ambao ulisababisha mji huo kukabidhiwa China kwamba "hauna maana tena".
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Sylvia Mwehozi