Xi awasili Serbia kituo cha pili cha ziara yake Ulaya
8 Mei 2024Ndege yake ilitua kwenye mji mkuu wa Serbia, Belgrade, ikisindikizwa na ndege za kivita chapa MIG-29 huku ulinzi ukiwa umeimarishwa. Xi alilakiwa na Rais Aleksandar Vucic kwa heshima ya zulia jekundu na gwaride la kijeshi na hivi leo viongozi hao wawili wanatarajiwa kufanya mazungumzo.
Xi anatazamiwa kujadili mpango wa uwekezaji wa mabilioni ya dola kwenye nchi hiyo inayozingatiwa na China kuwa mshirika muhimu kwenye kanda ya Balkani.
Ziara ya Xi inafanya sambamba na kumbukumbu ya miaka 25 ya kushambuliwa ubalozi wa China mjini Belgrade kulikofanywa na ndege za kivita za NATO.
Jengo hilo lililengwa Mei 7, 1999 wakati wa operesheni ya NATO ya kumlazimisha kiongozi wa wakati huo wa Serbia, Slobadan Milosevic kukomesha hujuma zake za kujaribu kuzima uasi wa jimbo la Kosovo.