1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Xi achaguliwa tena kukiongoza chama cha kikomunisti China

25 Oktoba 2017

Rais wa China Xi Jinping ametangaza safu mpya ya uongozi wa kamati kuu ya chama tawala cha kikomunisti, wakati akianza muhula mpya wa miaka mitano, akilenga kuimarisha ustawi na kupanua ushawishi wa taifa hilo kimataifa.

China Xi Jingping
Picha: Getty Images/W.Zhao

Kama ilivyotarajiwa, Xi amepewa muhula mwingine, kufuatia mkutano wa kwanza wa kamati kuu mpya iliochaguliwa wakati wa mkutano mkuu wa chama unaofanyika mara mbili katika muongo mmoja.

Chama hicho tayari kilipandisha hadhi ya Xi siku ya Jumanne, wakati wa kikao cha kuhitimisha mkutano huo, kwa kuliingiza jina lake na itikadi yake katika katiba ya chama, sambamba na viongozi waliopita - Mao Zedong na Dang Xiaoping, na hivyo kumfanya kuwa kiongozi mwenye nguvu zaidi wa taifa hilo katika kipindi cha miongo kadhaa.

Hatua hiyo inafanya kitendo chochote cha kupingana naye kuwa shambulizi kwa chama chenyewe, na hivyo kumkinga kwa kiasi kikubwa dhidi ya  ushindani miongoni mwa makundi hasimu ya chama.

Xi alisema kurejea kwake kama Katibu Mkuu kunamaanisha siyo tu kukubalika kwa kazi yake, lakini pia kutiwa moyo kutakaomchochea kuendelea. "Katika muktadha huu mpya, tunapaswa kupata muonekano mpya, na muhimu zaidi, kufanikisha mambo mapya," alisema wakati akizungumza na waandishi habari katika ukumbi wa watu kutambulisha kamati hiyo mpya.

Wajumbe wa kamati kuu mpya ya chama cha kikomunisti, ambayo ndiyo chombo kikuu cha maamuzi cha taifa hilo. (Kushoto-Kulia) Han Zheng, Wang Huning, Li Zhanshu, Rais wa China Xi Jinping, waziri mkuu Li Keqiang, Wang Yang, Zhao Leji wakikutana na waandishi habari Oktoba 25,2017.Picha: Getty Images/W.Zhao

 

Uwakilishi wa kamati

Muundo wa Kamati Kuu mpya ya chama cha Kikomunisti, yenye wajumbe saba, unaakisi juhudi za Xi kuimarisha umoja, kwa kuweka urari kati ya makundi yenye maslahi tofauti katika chama hicho chenye wanachama milioni 89, mnamo wakati akitafuta kukiweka katika nafasi nzuri ya kudhibiti masuala ya China ndani na nje.

Mjumbe pekee alierejea kwenye kamati hiyo ni waziri mkuu Li Keqiang, afisa wa pili wa ngazi ya juu mwenye jukumu la kusimamia uchumi na kuongoza baraza la mawaziri.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo kulingana na mpangilio wa ukuu ni Li Zhanshu, mkurugenzi wa ofisi kuu ya chama ambaye pia ni mkuu wa shughuli za ofisi ya rais, Naibu Waziri Mkuu Wang Yang; Wanga Huning, mkurugenzi wa ofisi kuu ya utafiti ya chama; Zhao Leji, mkuu wa shirika linalohusika na utoaji kazi; na kiongozi wa chama katika mkoa wa Shanghai Han Zheng.

Mchuuzi wakionyehsa hedaya yenye picha za rais wa Cina Xi Jinping (kushoto) na hayati mwenyekiti wa China Mao Zendong (kulia), kwa wageni nje ya Ukumbi Mkuu wa Watu ambako mkutano mkuu wa chama ulifanyika.Picha: Getty Images/Feng Li

Malengo yenye makuu

Xi ameifanya kampeni pana dhidi ya rushwa kuwa sifa bainifu ya mhula wake wa kwanza madarakani. Wakati kampeni hiyo ni maarufu miongoni mwa raia wa kawaida, baadhi wanaiona kama mbinu ya kuwaondoa mahasimu wake na wapinzani wa kisiasa ili aweze kuimarisha udhibiri wake wa chama kwa ngazi zote.

Sambamba na kampeni hiyo, XI amesimamia ukandamizaji mkali dhidi ya asasi za kiraia, unaolenga kuzima upinzani na harakati miongoni mwa mawakili na watetezi wa haki.

Xi ameainisha dira yake ya kuimarisha jukumu la chama katika maisha ya Wachina na kulijega taifa hilo kuwa dola lenye nguvu zaidi katika wakati ambapo Marekani na mataifa mengine ya Magharibi yakionekana kurudi nyuma.

Mtoto huyo wa mzee masikini  wa kikomunisti, ameielezea itikadi yake ya kisiasa kama nguzo ya kuiweka China kwenye njia ya kuwa taifa kubwa la kisasa la Kisoshalisti, kufikia katikati ya karne hii.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,dpae.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman