1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiAsia

Xi Jinping: Mradi wa BRI uko katika mwelekeo sahihi

Angela Mdungu
18 Oktoba 2023

Rais wa China Xi Jinping amesema mradi mkubwa wa miundombinu ya barabara na Reli, BRI uko katika njia sahihi licha ya mivutano na mizozo ya kimataifa.

Rais Xi Jinping akihutubia mkutano wa BRI
Rais Xi Jinping akihutubia mkutano wa BRIPicha: Ng Han Guan/AP/picture alliance

Kulingana na rais Xi Jinping, mataifa yanayoendelea yanatakiwa pia kunufaika na mradi huo wa miundombinu ya barabara na reli ulioanzishwa miaka 10 iliyopita, akisema mabadiliko ya kihistoria sasa yanaonekana kote ulimwenguni. Miongioni mwa wawakilishi kutoka mataifa zaidi ya 140 alikuwa rais Vladimir Putin wa Urusi.

Soma zaidi: Putin akutana na mwenyeji wake Xi Jinping katika mkutano wa mradi wa BRI mjini Beijing

Kwenye hotuba yake hii leo, Xi aliikosoa Marekani na mataifa ya Umoja wa Ulaya kama Ujerumani ambayo si wanachama wa mradi huo, lakini yameliwekea vikwazo taifa hilo ama kuzichunguza bidhaa zake na kuongeza kuwa vikwazo hivyo vya upande mmoja, vinazuwia ukuaji wa kiuchumi na kuvuruga mifumo ya ugavi.

Putin aliyezungumza baada ya Xi alianza kwa kuisifu BRI akisema mradi huo na ushiriki wa Urusi vimesaidia kupata suluhu ya pamoja katika masuala mbalimbali ya kikanda. Uwepo wa Putin kwenye mkutano huo ni ishara ya wazi kwamba Urusi itasalia kuwa mshirika wa karibu sana wa Beijing.

Baadhi ya washiriki wamtenga Putin

Hata hivyo baadhi ya wawakilishi wa mataifa ya magharibi walitoka wakati Putin alipokuwa akihutubia. Hii ni baada ya mataifa mengi kumtenga kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine. Lakini pamoja na hayo, Xi amemuhakikishia ushirikiano zaidi Putin, walipokutana katika mkutano baina yao.

Rais Vladmir Putin wa Urusi akiwa na Rais Xi Jin Ping wa ChinaPicha: Sergei Guneyev/Pool/picture alliance

Katika hatua nyingine, Rais wa Sri Lanka Ranil Wickremesinghe amesema unafuu wa madeni katika nchi za kipato cha chini unapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko kuelekea uchumi wa kijani. Amesema kuwa kutokuchukua hatua katika suala la madeni kunaweza kuwa kitisho kikubwa kwa mradi wa miundombinu ya barabara na reli.

Rais huyo wa Sri Lanka amesema mpango wa ustawi wa hali ya hewa wa nchi yake unahitaji uwekezaji wa dola za Kimarekani bilioni 26.5 hadi kufikia mwaka 2042 na mkakati wa kutekeleza sera ya kuondoa hewa ya ukaa utapaswa kutumia dola bilioni 100 kufikia mwaka 2050.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW