Japan na China zakubaliana kuimarisha ushirikiano
17 Novemba 2023Xi na Kishida walifanya mazungumzo pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Mataifa ya Asia na Pasifiki, APEC mjini San Francisco, nchini Marekani.
Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida alisema hayo mbele ya waandishi wa habari baada ya mazungumzo marefu baina yake na Xi jana usiku. Viongozi hao wawili pia walijadiliana juu ya zuio la China la bidhaa za baharini kutoka Japan pamoja na kesi inayomuhusisha mfanyabisara mkubwa wa Japan anayezuiwa nchini China.
Hivi karibunio, uhusiano baina ya mataifa hayo mawili uliingia doa baada ya China kuzuia bidhaa za baharini kutoka Japan kufuatia uamuzi wa Japan wa kuyatiririsha maji yaliyosafishwa na kuondolewa viambata vya mionzi kutoka kinu cha nyuklia cha Fukishima kilichoharibiwa na tetemeko kubwa la ardhi, kuelekea kwenye Bahari ya Pasifiki, katika operesheni ya mwezi Agosti ambayo Japan ilisisitiza kuwa ilikuwa salama.
Japan yaielezea China juu ya mashaka ya usalama wa Taiwan
Kishida, amesema amemuhimiza Xi kuondoa zuio hilo, huku pia akiibua masuala mengine na hasa wasiwasi wake mkubwa juu ya msururu wa masuala ya kidiplomasia na kijeshi kuanzia mzozo wa visiwa vya Senkaku hadi mvutano kati ya China na kisiwa cha Taiwan ambacho inadai ni himaya yake.
"Nilielezea wasiwasi wangu mkubwa kuhusiana na shughuli za pamoja za kijeshi katika ya China na Urusi karibu na eneo la bahari la Japan na kusisitiza kwamba ni muhimu kwa jamii ya kimataifa ikiwa ni pamoja na Japan kuhakikisha amani na utulivu kote katika Ujia wa Taiwan," alisema Kishida.
Viongozi hao wamekubaliana kufanya mazungumzo ya ngazi za juu kujadiliana masuala ya kiuchumi na kukaribisha hatua ya kuanzishwa kwa mpango kazi mpya wa kuangazia udhibiti wa mauzo ya nje kwa kuzingatia maslahi ya mataifa yote mawili.
Xi kwa upande wake aliitaka Japan kulichukulia suala la maji ya Fukushima kwa umakini mkubwa na pande hizo mbili zilikubaliana kujaribu kusuluhisha kwa mazungumzo, hii ikiwa ni kulingana na muhtasari wa mazungumzo hayo. Hata hivyo China haikuzungumzia kisa cha mfanyabiashara huyo wa Japan iliyomkamata mwezi uliopita kwa madai ya ujasusi.
Soma zaidi: Mkutano wa kilele wa APEC wafanyika tena Marekani baada ya zaidi ya miaka 10
Katika hatua nyingine, Rais Joe Biden wa Marekani na Rais wa Mexico Andres Manuel Lopez Obrador wanataraji kukutana baadae leo mjini San Francisco kujadiliana juu ya majanga ya uhamiaji kwenye mpaka baina ya mataifa hayo, pamoja na dawa za kulevya aina ya fentanyl.
Marekani na China washindaniana washirika zaidi katika mkutano wa APEC
Mazungumzo ya wakuu hao pembezoni mwa mkutano huo wa kilele wa APEC yanafanyika wakati masuala hayo mawili yakitarajiwa kuugubika pakubwa uchaguzi ujao wa Marekani wakati Biden akiisaka awamu ya pili.
Mara ya mwisho kwa marais hao kukutana ilikuwa ni mwezi Januari katika mkutano wa kilele wa viongozi wa Amerika ya Kaskazini uliofanyika Mexico. Rais Xi Jinping wa China aliahidi wakati alipokutana na Biden siku ya Jumatano kuchukua hatua kali dhidi ya wazalishaji wa viungo vya fentanyl nchini mwake, wakati dawa hizo zikiendelea kumiminika nchini Marekani.
Huku hayo yakiendelea, Biden na Xi wamejikuta wakishindania washirika wa ushirikiano huo wa APEC katika mkutano wao unaoe ndelea, siku moja baada ya viongozi hao wawili kukutana katika azma ya kupunguza mvutano kati ya mataifa hayo makubwa kiuchumi, ambapo waliahidi kuimatisha ushirikiano wa kijeshi, miongoni mwa mengineyo.
Biden amesisitiza mbele ya mataifa hayo kwamba ushirikiano thabiti kati ya Marekani na China sio tu ni muhimu kwa mataifa hayo mawili bali pia kwa ulimwengu mzima.
China na Marekani wanashindana kuongeza ushawishi katika eneo lote kuanzia pwani za Canada, hadi Chile na kote nchini Australia, Malaysia na Urusi, wakati China ikiwa inasaidia ujenzi wa miundombinu na mikopo kupitia programu yake ya Belt and Roads, Marekani imekuwa ikijaribu kuimarisha ushirikiano wa kiabiashara na makubaliano mengine.