1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Xi na Putin kukutana katika mkutano wa SCO, Uzbekistan

15 Septemba 2022

Rais wa China Xi Jinping na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wapo, Uzbekistan kwa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) iliyoundwa na China na Moscow kupambana na ushawishi wa Marekani duniani.

China Peking | Wladimir Putin und Xi Jinping Februar 2022
Picha: Alexei Druzhinin/AP/picture alliance

Mkutano huo wa kilele wa Mataifa manane yanayounda Jumuiya ya ushirikiano wa Shanghai SCO ikiwa ni pamoja na China, Urusi, India, Pakistan na mataifa manne ya Asia ya Kati ambayo ni Kazakhstan, Kyrgyzstan, Uzbekistan na Tajikistan, unakuja wakati Rais wa Urusi Vladimir Putin anaendelea kutengwa na mataifa ya Magharibi kufuatia hatua yake ya kuivamia Ukraine kijeshi. Mkutano huo pia unafanyika wakati uhusiano wa China na Marekani, Ulaya, Japan na India unayumba kutokana na mizozo juu ya teknolijia, Usalama na maeneo yanayozozaniwa.

Xi alilakiwa katika uwanja wa ndege wa Samarkand na rais wa Uzbekistan Shavkat Mirziyoyev. Ziara hii ni ya kwanza kwa rais huyo wa China tangu kuripuka kwa janga la corona miaka miwili na nusu iliyopita hali iliyotatiza nguvu za Beijing kutaka kutanua mbawa zake kama taifa muhimu na lililo na nguvu kikanda.

Kulingana na mshauri wa Rais wa Urusi, baadae Xi na Putin watakutana ana kwa ana kwa mazungumzo juu ya Ukraine. Waziri Mkuu Narendra Modi anatarajiwa kufika Samarkand leo Alhamisi lakini hakuna dadlili zozote zinazoonesha iwapo atakutana pembezoni mwa mkutano huo na Xi au Putin.

Mahusiano ya China na India yanayumba kufuatia mapambano kati ya wanajeshi wa mataifa hayo mawili katika mgogoro eneo la Mpaka wa Gogra kwenye milima ya Himalaya.

Xi anataka kuimarisha mpango wake wa usalama duniani

Rais wa China Xi JinpingPicha: Ng Han Guan/AP Photo/picture alliance

Hata hivyo katika mkutano huu kiongozi wa China anataka kuuimarisha mpango wa usalama duniani uliotangazwa mwezi Aprili kufuatia Marekani kuunda kundi la Quad linalowajumuisha viongozi wa mataifa manne ya India-Pasifiki, ambayo ni Japan India na Australia ili kujibu sera kali za kigeni zilizowekwa na Beijing.

Xi bado hajatoa maelezo yoyote juu ya mpango huo wa usalama wa dunia lakini tayari maafisa wa Marekani wanalalamika wakisema unatetea hoja za Urusi na kuunga mkono uvamizi wa taifa hili nchini Ukraine. Eneo la Asia ni sehemu ya mradi mkubwa wa china wa ujenzi wa miundombinu ya usafiri na barabara unaojulikana kama Belt and Road Initiative unaonuiwa kutanua biashara kuanzia Asia pasifiki, Mashariki ya Kati, Ulaya na Afrika.

Hatua ya China kutaka kutanua mbawa zake kiuchumi ndani ya Asia ya Kati kunaipa wasiwasi Urusi inaloliona eneo hilo kama nyanja yake ya ushawishi. Kazakhstan nayo pamoja na jirani zake zinajaribu kuivutia China kiuwekezaji lakini ikiwa makini kutoikasirisha Moscow.

Chanzo: afp,ap