Xi: Uhusiano wa China na Urusi ndio thabiti zaidi duniani
26 Agosti 2025
Xi amesema hayo kwenye mazungumzo na Mwenyekiti wa Bunge la Urusi Vyacheslav Volodin na kuendelea kuusifia uhusiano huo alioutaja kama "chanzo thabiti cha amani ya ulimwengu," hii ikiwa ni kulingana na shirika la utangazaji la serikali ya China, CCTV.
Uhusiano kati ya washirika hao wa zamani wa kisoshalisti na wenye historia ndefu, umeimarika tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mnamo Februari 2022 na China haijawahi kulaani uvamizi wa Urusi nchini humo. Lakini China inasisitiza kwamba inasimama katikati na haiegemei upande wowote.
Rais Putin pia anatarajiwa kuzuru China mwishoni mwa wiki hii na atahudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Usalama ya Shanghai, CSO katika mji wa Tianjin, kuanzia Agosti 31 hadi Septemba Mosi, pamoja na maadhimisho ya miaka 80 ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia. Atafanya pia mazungumzo na Xi.
Kellog: Marekani yasaka kwa nguvu dhamana ya usalama ya Ukraine
Mbali na hayo habari kutoka mjini Kyiv zinasema, mjumbe maalumu wa Rais Donald Trump wa Marekani, Keith Kellog alisema jana Jumatatu akiwa mjini humo kwamba maafisa wa Marekani wanafanya juhudi kubwa sana za kumaliza vita vya nchini Ukraine vilivyodumu kwa miaka mitatu, katikati ya mashaka makubwa ya kupatikana suluhu.
Amesema kikubwa kinachohangaikiwa sasa ni kupatikana kwa dhamana ya usalama kwa ajili ya Ukraine, ambayo inahofu huenda akavamiwa kwa mara nyingine na Urusi. Amesema hayo baada ya kushiriki Ibada ya Kitaifa ya Mwaka, sambamba na wanasiasa, wafanyabiashara na wanadiplomasia.
Kwa upande wake, Naibu Kansela wa Ujerumani Lars Klinbeil, yeye amesema anataka kufahamu zaidi "matarajio" ya Rais Zelenskyy kuelekea suala hilo la dhamana ya usalama wakati wa ziara yake mjini Kyiv jana Jumatatu.
Lars Klinbeil na ujumbe wake walikutana na maafisa wa Ukraine kujadili "jinsi gani Ujerumani inaweza kuiunga mkono Ukraine katika mchakato wa amani."
"Pia nina hamu ya kusikia matarajio yako kuhusu dhamana ya usalama, hasa kutokana na hali ilivyo sasa. Ningependa kuliibua hili katika mijadala ya Wajerumani. Hata hivyo, ninaamini pia, na hii itakuwa ni hoja yangu ya mwisho hapa, kwamba lazima tujadili nini kitatokea ikiwa Rais (Vladimir) Putin hatakubali, ikiwa anataka kuendeleza vita."
Na kwenye uwanja wa vita, Urusi imepunguza shughuli kwenye viwanja vya ndege kadhaa nchini humo usiku kucha wa jana, kutokana na mashambulizi ya droni ya Ukreni kwenye anga zake. Miongoni mwa viwanja vilivyoathirika ni uwanja wa ndege wa Pulkovo huko St. Petersburg, mamlaka ya usafiri wa anga ya shirikisho imesema.