1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Angela Mdungu Mhariri: BruceAmani
16 Februari 2024

Yaliyomo katika magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika wiki hii: Mgogoro wa Kenya na Uganda umeangaziwa, uwepo wa majasusi wa Ukraine barani Afrika umemulikwa, shambulio la hivi karibuni mjini Mogadishu pia limegusiwa.

William Ruto, Rais wa Kenya katika moja ya hotub zake
Rais wa Kenya, William RutoPicha: Khalil Senosi/AP/picture alliance

Kati ya yaliyoandikwa na magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika wiki hii ni pamoja na Mgogoro wa Kenya na Uganda, Uwepo wa majasusi wa Ukraine barani Afrika na shambulio la hivi karibuni lililoutikisa mji mkuu wa Somalia,  Mogadishu.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung wiki hii liliandika kuhusu mgogoro kati ya Uganda na Kenya likiwa na kichwa cha habari kinachosomeka, "Maslahi ya kibiashara yana nguvu zaidi kuliko urafiki”

Habari hiyo inaanza kueleza kuwa, William Ruto amekuwa Rais wa Kenya chini ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu. Yoweri Museveni Rais wa Uganda wa miaka 38, anadaiwa kuwa mshauri na msaada katika ushindi wa Ruto kwenye uchaguzi wa mwaka 2022. Pamoja na hayo, uhusiano kati ya nchi hizo mbili za Afrika ya mashariki ambazo ni majirani haujawahi kuwa mbaya kama ulivyo hivi sasa.

die tageszeitung linakwenda mbali zaidi na kusema, hata nyakati za utawala wa nduli Idi Amin mwaka 1971 hadi 1979, mara zote, Uganda ilifanikiwa kumaliza tofauti zake na Kenya haraka na kimya kimya.

Sababu ya mgogoro unaoendelea sasa ni mafuta. Uganda inaagiza mafuta kutoka Kenya kwa takriban gharama ya dola za kimarekani bilioni mbili kila mwaka kupitia bandari ya Mombasa. Mafuta hayo hununuliwa na wafanyabiashara wa Kenya wanaopata faida kubwa kwa kuyauza Uganda. Lakini sasa, Uganda inataka kununua mafuta yake yenyewe moja kwa moja, bila ya wafanyabiashara wa Kenya na hivyo kufanya bidhaa hiyo kuwa ya bei nafuu kwa Uganda.

Gazeti hilo linaeleza kuwa, mwaka uliopita, kampuni ya mafuta ya serikali ya Uganda iliomba leseni ya kusafirisha mafuta. Kwakuwa Rais Ruto na Museveni walikuwa marafiki wa karibu,  maombi hayo yalionekana kuwa ni suala la kufuata utaratibu tu. Lakini Kenya iliweka masharti makali. Wafanyabiashara wa mafuta wa Kenya walikwenda mahakamani na walishinda zuio dhidi ya utoaji wa leseni kwa Uganda.

WELT plus

Welt Plus, liliandika kuhusu uwepo wa maafisa wa Shirika la Ujasusi la Ukraine barani Afrika. Limeandika, moja ya video iiliyoibuka hivi karibuni inaendelea kuchochea fununu kuhusu shughuli za Ukraine barani Afrika. Video hiyo yenye urefu wa sekunde 82 inasemekana kuonesha wapiganaji mamluki wa kampuni binafsi ya Wagner ya Urusi wakikamatwa huko Sudan. Jumatatu, Gazeti la Kyiv Post lilichapisha sehemu ya picha kutoka kwenye video hiyo inayodaiwa kuonesha mamluki waliokamatwa wakihojiwa na majasusi wa Ukraine.

Welt Plus linaendelea kuandika kuwa Kiev inashirikiana na jeshi la nchi hiyo katika mapambano yake dhidi ya wanamgambo wa RSF wanaoungwa mkono na Wagner hatua inayolibana kundi hilo la kampuni ya nchini Urusi. Ikiwa uvumi kuhusu video itathibitika kuwa ni ya uhakika, huu unaweza kuwa ushindi mkubwa kwa Ukraine.

Zeit Online

Gazeti la Zeit Online wiki hii lililimulika  Shambulio mjini Mogadishu ambalo limewauwa watu 18 na limewajeruhi wengine 28. Kulingana na taarifa ya jeshi, shambulio hilo lilifanywa Jumamosi katika kambi ya jeshi. Kati ya waliouwawa ni wakufunzi sita wa jeshi kutoka Falme za Kiarabu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa mwanamume mmoja aliyevalia sare za jeshi alianza kuwamiminia risasi wakufunzi wa jeshi wa kigeni na wenyeji. Msemaji wa polisi alisema pia kuwa, watu wengine waliuwawa pia msikitini wakati wa sala ya jioni.

Vikosi vya usalama vikishika doria baada ya shambulio la Februari 21.2023Picha: Hassan Ali ELMI/AFP

Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa, mwanachama wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab alifanikiwa kujipenyeza na kusajiliwa kama mmoja wa waliosajiliwa kupata mafunzo hay. Kundi hilo kupitia redio yake limekiri kuwa limehusika na shambulio hilo na kujitapa kwamba limewauwa mamluki wa kigeni.  Amri ya kutokutoka nje ilitangazwa baada ya tukio hilo katika sehemu kubwa ya Mogadishu. Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud alizungumzia shambulizi hilo la kikatili na kuongeza kuwa uchunguzi unafanyika.

die tageszeitung

die tageszeitung limegusia kuhusu kinachoendelea Senegal. Mhariri ameandika, vikosi vya usalama vya Senegal vinatumia nguvu kubwa kuzuia maandamano dhidi ya hatua ya kufutwa kwa uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 25.

Jumanne jioni katika mji wa Saint Louis ulio kaskazini mwa Senegal karibu na mpaka wa Mauritania, vijana walikusanyika kukabiliana na vikosi vya usalama. Wanausalama hao walishajiweka tayari katika maeneo kadhaa wakati wa mchana kuzuia maandamano yasisambae.

Maandamano mengine yalitangazwa Jumanne dhidi ya hatua hiyo ya Rais Macky Sall ya kuuahirisha uchaguzi wa Rais. Katika mji mkuu Dakar, maandamano yalipigwa marufuku dakika ya mwisho. Hata hivyo chama kipya cha kiraia cha "Aar Sunu Election”  maneno yanayomaanisha linda katiba yetu, kimeitisha maandamano mapya Jumamosi.

FAZ.NET

Magazeti kadhaa ya hapa Ujerumani likiwemo gazeti la mtandaoni la Faz.net yaliandika kuhusu habari ya majonzi ya kifo cha mwanariadha wa Kenya Kelvin Kiptum aliyefariki dunia kwa ajali ya gari. Faz.net Limemnukuu kamanda wa polisi Peter Mulinge, wa  Elgeyo Marakwet aliyethibitisha taarifa hiyo akisema kuwa  mwanariadha huyo aliyekuwa akishikilia rekodi ya dunia ya mbio za Marathon alifariki Jumapili usiku akiwa na kocha wake Gervais Hakizimana.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW