1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yamal aendeleza burudani Barcelona

2 Machi 2026

Nyota wa Barcelona, Lamine Yamal, aandika historia kwa kufunga "hat trick" yake ya kwanza katika taaluma yake wakati walipolaza Villarreal mabao 4-1 na kujikita kileleni mwa msimamo wa La Liga kwa tofauti ya pointi nne.

Champions League 2025 | FC Barcelona vs. Olympiacos Piräus | Lamine Yamal am Ball
Picha: Matthieu Mirville/firo Sportphoto/picture alliance

Akiwa na umri wa miaka 18 na siku 230, Yamal ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga hat trick yake ya kwanza katika La Liga, kwa mujibu wa takwimu za Opta. Bao lake la pili lilikuwa la kuvutia zaidi baada ya kupenya kutokea wingi wa kulia, kumpita beki mmoja na kupiga shuti kwa ustadi na kutinga kona ya mbali.

Kocha wa Barcelona, Hansi Flick, alimpongeza winga huyo akisema ni mchezaji wa kipekee anayewafurahisha mashabiki, huku akisisitiza kuwa bado ana nafasi kubwa ya kuendelea kukua na kuboresha kiwango chake licha ya umri mdogo.

Bao la nne la Barcelona lilifungwa dakika za nyongeza na mshambuliaji mkongwe Robert Lewandowski, ambaye aliingia akitokea benchi.

Hata hivyo, ushindi huo ulighubikwa na habari mbaya kwa Barcelona baada ya kuthibitishwa kuwa Lewandowski amevunjika mfupa wa tundu la jicho la kushoto kufuatia jeraha alilopata katika mchezo huo dhidi ya Villarreal. Kutokana na hali hiyo, atakosa mechi ya nusu fainali ya Copa del Rey dhidi ya Atlético Madrid.

Barcelona, ambao ni mabingwa watetezi wa Copa del Rey, walipokea kipigo cha mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza dhidi ya kikosi kinachonolewa na Diego Simeone mapema Februari, hali inayofanya mechi ya marudiano kuwa na presha kubwa kwa miamba hao wa Catalonia.

Lewandowski, mwenye umri wa miaka 37, amekuwa na nafasi ndogo msimu huu, mara nyingi akiachwa benchi huku Ferran Torres akipewa kipaumbele katika safu ya ushambuliaji. Pamoja na hilo, uzoefu wake umekuwa muhimu katika nyakati za maamuzi.

Wakati Barcelona wakijikita kileleni mwa La Liga, wapinzani wao wa karibu Real Madrid CF wana nafasi ya kupunguza pengo la pointi endapo watashinda mechi yao inayofuata, huku ushindani wa ubingwa ukizidi kupamba moto.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW