Yanayojiri Ukraine: Mashambulizi yaripotiwa Belgorod
23 Mei 2023Gavana wa jimbo la Belgorod lililoko Urusi Vyacheslav Gladkov amesema kupitia mtandao wa Telegram kwamba Wizara ya Ulinzi na vyombo vingine vya usalama vinafanya operesheni katika eneo hilo. Ameongeza kuwa japo hakuna maafa ambayo yameripotiwa kufikia sasa, ni mapema sana kwa wakaazi kurejea huko.
Maafisa wawili wa usalama wa kujitolea wakiwemo raia wa Urusi wanaoegemea upande wa Ukraine, walidai kuhusika na shambulizi hilo. Kwamba walitaka kuunda eneo lisilo na shughuli za kijeshi mpakani humo ili kuzuia jeshi la Urusi kuishambulia Ukraine. Ukraine imekanusha kuhusika na operesheni hiyo. Kulingana na Gladkov, kikosi cha ujasusi na hujuma kiliingia katika eneo hilo.
Urusi yadai Ukraine imehusika kushambulia eneo lake la mpakani la Belgorod
"Kuna habari kwamba raia wawili wamejeruhiwa katika maeneo ambako adui ameingia. Hadi sasa vikosi vya usalama havijaweza kuwafikia, na hilo ndiyo lilikuwa jukumu lao la kwanza. Ninatumai tutaweza kuwaondoa haraka iwezekanavyo na wapelekwe watibiwe. Hadi sasa hakuna vifo,” amesema Gladkov.
Kutokana na shambulizi hilo, Urusi imesema mapema Jumanne kwamba imeanzisha uchunguzi dhidi ya kile ilichokiita ‘ugaidi', na kwamba vikosi vyake vinakabiliana na kundi la hujuma ambalo limevuka mpaka kutoka Ukraine.
Kwenye taarifa, Kamati ya Uchunguzi ambayo aghalabu huchunguza matukio makubwa imesema imeanzisha uchunguzi wa jinai kuhusiana na shambulizi katika jimbo la Belgorod.
Wapiganaji wa kundi la Wagner wajiandaa kuondoka Bakhmut
Katika mapigano ya kuudhibiti mji wa Bakhmut, naibu waziri wa ulinzi wa Ukraine Hanna Maliar amesema leo kwenye mtandao wa Telegram, kwamba mapambano yamepungua kidogo lakini mashambulizi ya makombora yanaendelea mjini humo, na kwamba vikosi vyake vinadhibiti eneo dogo huku vikosi vya Urusi vikisafisha maeneo wanayoshikilia.
Urusi husema kuukamata mji wa Bakhmut kutafungua njia kuwezesha vikosi vyake kusonga mbele zaidi katika jimbo la mashariki mwa Ukraine Donbas, linalopakana na Urusi.
Hayo yakijiri rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, mapema Jumanne amevitembelea vikosi vyake vilivyo kwenye uwanja wa mapambano eneo la Donetsk mashariki mwa nchi hiyo, ambako Urusi imezidisha juhudi zao kutaka kuchukua udhibiti wake.
Taarifa kutoka ikulu ya rais mjini Kiev imesema, Rais Zelensky amezuru eneo hilo baada ya ziara yake ya kigeni. Amevitembelea vikosi vya Ukraine vinavyoimarisha ulinzi katika eneo la Vugledar-Maryinka huko Donetsk
(VYANZO: DPAE, RTRE, AFPE)