1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yanga, Simba zayaaga mashindano ya Klabu Bingwa Afrika

6 Aprili 2024

Klabu mbili za soka za nchini Tanzania, Yanga na Simba zimeyaaga mashindano ya klabu bingwa barani Afrika baada ya kupoteza michezo ya duru ya pili ya robo fainali.

Wachezaji wa Yanga
Wachezaji wa Yanga Picha: Young Africans

Timu ya Yanga ilikufa kibabe baada ya kuilazimisha klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kutafuta ushindi kupitia mikwaju ya penalti.

Sundowns walijikatia tiketi ya kucheza nusu fainali kwa kupachika wavuni penalti 3-2 za Yanga katika mchezo wa duru ya pili wa robo fainali uliopigwa mjini Pretoria.

Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bila kufungana kama iliyokuwa kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa mjini Dar es Salaam mwishoni mwa juma lililopita. 

Mlinda mlango wa Mamelodi, Ronwen Williams, alisadifu kuwa shujaa wa mchezo huo baada ya kuipangua mikwaju iliyopigwa na vijana machachari wa Yanga, Stephane Aziz Ki na Dickson Job.

Williams ambaye pia anaidakia timu ya taifa  alionesha uwezo kama ilivyokuwa miezi miwili iliyopita pale alipookoa mikwaju minne ya penalti wakati wa mtanange wa robo fainali ya mashindano ya soka ya mataifa ya Afrika ulioikutanisha Bafana Bafana na Cape Verde nchini Ivory Coast.

Mamelodi na mchezo usio na maajabu, VAR yaipokonya Yanga tonge mdomoni 

Mamelodi Sundowns walipochukua kikombe cha klabu bingwa barani Afrika mwaka 2016Picha: Ahmed Gamil/AP Photo/picture alliance

Mamelodi Sundowns ambao hawakuonesha mchezo wa kushangaza, sasa watasubiri kufahamu iwapo watacheza nusu fainali dhidi ya ama ASEC Mimosa ya Ivory Coast au miamba Eseperance ya Tunisia zitakazokutana leo mjini Abidjan.

Kwa ujumla Sundowns walitawala mchezo wote wa Ijumaa usiku lakini hawakuwa na umakini wa kuamua ni wakati gani hasa walipaswa kushambulia. Hali hiyo haikumnyima usingizi mlinda mlango wa Yanga Djigui Diarra.

Baada ya kipindi cha kwanza kilichoshuhudia shambulizi moja tu la uhakika kutoka kwa Sundowns, vijana wa Yanga walianza kuonesha makeke na hasa kasi ya mshambuliaji raia wa Burkina Faso Stephane Aziz Ki iligeuka kitisho cha wazi. 

Dakika 59 Ki aliamini ameipatia Yanga nafasi ya kusonga nusu fainali pale mkwaju wake mkali ulipompiga golikipa Williams na kugonga kingo ya ndani ya goli. Hata hivyo teknolojia ya VAR iliamua kwamba halikuwa goli.

Simba yaambulia kichapo kutoka kwa Al Ahly bila kupapatua 

Kikosi cha Klabu ya Simba Picha: BackpagePix/empics/picture alliance

Ulikuwa usiku mbaya kwa Tanzania pale klabu ya Simba nayo ilipokwaa kisiki kusonga mbele michuano ya klabu bingwa.

Simba walikubali kichapo cha bao 2-0 mbele ya miamba Al Ahly ya Misri mjini Cairo. Juma lililopita Simba pia iliambulia kipigo cha goli 1-0 katika duru ya kwanza ya robo fainali iliyopigwa mjini Dar es Salaam.

Amr el Solia ndiye aliipatia Al Ahly bao la kwanza mnamo dakika ya 47. Mahmoud Kahraba aliongeza la pili kupitia mkwaju wa penalti wakati wa dakika za nyongeza.

Al Ahly watacheza na mshindi wa mechi ya leo kati ya wenyeji Petro Luanda ya Angola na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.