Yanga yamtimua kocha licha ya kuendelea kushinda
7 Mei 2026
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Young Africans S.C. maarufu kama Yanga, wamemtimua kocha wao raia wa Ureno licha ya timu hiyo kuendelea kuongoza ligi bila kupoteza mchezo hata mmoja msimu huu.
Hatua hiyo imekuja baada ya Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC Jumatano, ushindi uliowasogeza karibu zaidi kutetea ubingwa wao wa tano mfululizo.
Katika taarifa fupi, klabu hiyo ilisema tu kuwa imeachana na Goncalves na kumshukuru kwa mchango wake ndani ya timu, bila kueleza sababu za kuondolewa kwake.
Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Angola alikuwa ameinoa Yanga kwa miezi saba pekee lakini aliisaidia kuendelea kuongoza ligi kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya watani wao Simba S.C.
Mbali na mafanikio ya ndani ya nchi, Goncalves pia aliiongoza Yanga kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya nne katika historia ya klabu hiyo, ingawa walishindwa kufika robo fainali.