Yellen asema Marekani haitakubali viwanda vipya kuharibiwa
8 Aprili 2024Yellen ameuambia mkutano na waandishi wa habari baada ya kukamilisha ziara ya siku nne ambapo alikutana na maafisa wa China kwamba mazungumzo baina yao yameimarisha maslahi ya Marekani.
Amesema, wakati soko la kimataifa likifurika bidhaa za bei nafuu za China, masoko ya Marekani na mataifa mengine ya kigeni yanaendelea kubaki mashakani.
"Hii ni aina ya mijadala tunayoifanya na mataifa mengine makubwa kiuchumi kwa vile tunajua kwamba suala la kifedha katika nchi ya kigeni linaweza kuingia kwa haraka nchini mwetu. Na nina furaha kwamba tunafanya vivyo hivyo na China.," alisema Yellen.
Amesema alizungumzia wasiwasi juu ya kupungua kwa mahitaji ya ndani ya China na uwekezaji uliopindukia kwenye viwanda kama vya magari ya umeme, betri na bidhaa za umeme wa jua, uliochochewa na ruzuku kubwa kutoka serikalini.