1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yemen itaporomoka iwapo hakutakuwa na ufadhili zaidi

25 Juni 2020

Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Mark Lowcock ameonya kuwa bila usaidizi mkubwa wa kifedha, Yemen itaporomoka, na watu wake wengi watafariki kutokana na baa la njaa, ugonjwa wa COVID-19, kipindupindu.

Schweiz | UN-Nothilfekoordinator Mark Lowcock | Klimawandel | Migration
Picha: picture-alliance/Keystone/S. Di Nolfi

Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa amekiarifu kikao cha faragha cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano kwamba ugonjwa wa COVID-19 unaenea kwa haraka kote nchini Yemen na takriban asilimia 25 ya watu waliothibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona wamefariki hiki kikiwa kiwango mara tano zaidi cha wastani wa dunia.

Mark Lowcock ameongeza kuwa huku mfumo wa afya ukiwa umesambaratika, wanafahamu kuhusu visa vingi ambavyo havijarekodiwa na kwamba gharama ya mazishi katika baadhi ya maeneo imeongezeka mara saba zaidi ikilinganishwa na miezi michache iliyopita.Ameendelea kusema kuwa janga la virusi vya corona linaoongeza masaibu yaliyoko ikiwa ni visa vya baadhi ya watu kuwa wahanga wa madhila mengi kwa wakati mmoja, huku uchumi wa nchi hiyo ukielekea katika hali mbaya ambayo haijawahi kushuhudiwa.

Lowcock alitaja kushuka kwa haraka kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo rial, mfumko wa bei kutoka asilimia 10 hadi 20  katika  bei za chakula katika muda wa wiki mbili pekee na takwimu zinazoonesha kuwa malipo huenda yamepungua kwa asilimia 50 na 70. Mkuu huyo wa huduma za kibinadamu za Umoja wa Mataifa amesema kuwa kongamano lililoandaliwa kwa njia ya video na Umoja wa Mataifa na Saudia Arabia kwa ajili ya Yemen mnamo Juni 2 lilishuhudia wafadhili 31 wakiahidi msaada wa dola bilioni 1.35 za msaada wa kibinadamu ikijumuisha ufadhili mpya wa takriban dola milioni 700.

Wanajeshi wa serikali watembea katika eneo la shambulizi la kombora, Marib YemenPicha: Reuters/A. Owidha

Mipango itakayoanza kufungwa kwa ukosefu wa ufadhili

Amesema kuwa kiasi hicho ni karibu na nusu ya kile kilichoahidiwa mwaka jana na chini ya kile kinachohitajika kuendeleza mipango ya misaada ya kibinadamu. Katika taarifa iliyosambazwa na afisi yake, Lowcock amesema kuwa kupungua kwa ahadi kutoka eneo la ghuba, kunachangia upungufu wote ulioko. Lowcock amesema kuwa mipango ya maji na usafi inayowahudumia watu milioni 4 itaanza kufungwa katika wiki kadhaa zijazo na  kiasi cha watoto milioni 5 watakosa chanjo zinazohitajika na kwamba kufikia mwezi Agosti, mipango ya kushughulikia utapiamlo pia itafungwa.

Ameongeza kwamba mpango mkubwa wa kiafya unaowasaidia watu milioni 19 pia utasitishwa. Kulingana na Lowcock, hawajawahi kushuhudia hali kama hiyo nchini humo ambapo kuna mzozo mkubwa wa kiuchumi pamoja na kupungua kwa kiasi kikubwa cha malipo na kupunguzwa kwa kiasi kikubwa cha misaada ya wafadhili  na kwamba haya yote yanatokea katikati mwa janga la virusi vya corona.

Lowcock amewahimiza wafadhili kugeuza ahadi zao kuwa katika mfumo wa kifedha na kuzingatia kuongeza kiwango hicho na pia makadirio ya ubadilishanaji wa sarafu za kigeni kuepukana na kuporomoka kwa uchumi. Lowcock ameongeza kuwa kuna chaguo gumu duniani kwasasa, aidha kuunga mkono msaada wa kibinadamu nchini Yemen na kusaidia kubuni fursa ya suluhisho la kisiasa la kudumu ama kuiangalia nchi hiyo ikiporomoka.

Siku ya Jumanne katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa kuongezwa kwa shinikizo dhidi ya pande zinazozozana nchini Yemen kuja pamoja na kupanga makubaliano ya kusitisha mapigano katika vita ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu elfu 10 na kupotea kwa makazi ya watu milioni 2 na pia kuchochea mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani. Guterres amesema kuwa Umoja huo umekuwa ukijaribu kuleta pande hizo pamoja na umekuwa ukishawishi mikakati ya kujenga imani inayojumuisha matumizi ya viwanja vya ndege, bandari, malipo ya mishahara na wakati huo huo mwanzo mpya wa mkakati wa kisiasa.