1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yemen: Mapigano yazuka tena Hodeida

Daniel Gakuba
20 Novemba 2018

Mapigano yamezuka tena baina ya waasi wa kihouthi na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, kuwania mji wa bandari wa Hodeida. Uhasama huu mpya umetokea wakati Umoja wa Mataifa ukihimiza juhudi mpya za amani.

Jemen Hodeida Kämpfer
Vita vya Yemen vimedumu kwa miaka 3, vikiuwa maelfu ya watu.Picha: picture-alliance/AP Photo/N. El-Mofty

Walioshuhudia kuibuka kwa mapigano hayo mapya, wamesema yamekuwa makali zaidi tangu wiki iliyopita, ambapo vikosi vya upande wa serikali vilisimamisha mashambulizi dhidi ya mji wa Hodeida ulio kwenye Bahari ya Sham. Vyanzo vya habari kutoka serikali ya Yemen vimesema mapambano hayo yameijikita Mashariki mwa mji huo, ambako wahouthi wamekuwa wakifyatua mizinga.

Vikosi vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia vimejibu kwa mashambulizi 12 ya kutumia ndege za kivita, hii ikiwa ni kwa mujibu wa duru hizo za upende wa serikali. Kumeripotiwa pia makabiliano ya bunduki katika mtaa wa Khamsin katikati mwa jiji la Hodeida, na katika wilaya ya al-Saleh. Mivutano hii mipya imefuatia ahueni ambaye imekuwepo tangu mwezi uliopita.

Wahouthi wavunja ahadi yao

Awali waasi wa kihouthi walisema walirusha makombora ndani ya Saudi Arabia, wakijibu walichokiita ''jaribio la kuingilia mipaka ya Yemen'' na mashambulizi ya anga. Saa chache kabla ya mashambulizi hayo, wahouthi walikuwa wametangaza kusitisha mashambulizi ya maroketi dhidi ya Saudi Arabia, ili kunusuru juhudi za kutafuta amani.

Watoto ni miongoni mwa wahanga wakubwa wa vita hivi vya YemenPicha: Getty Images/AFP/D. Souleiman

Tangu majira ya kiangazi, muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, ambao unaungwa pia mkono na Marekani umekuwa ukijaribu kuukomboa mji muhimu wa Hodeida kutoka mikononi mwa waasi, na vikosi vyake vimepiga kambi umbali wa kilomita 5 kutoka bandari ya mji huo, ambayo ni njia muhimu kwa mahitaji ya kibinadamu nchini Yemen.

Pigo kwa juhudi za Umoja wa Mataifa

Mapigano haya mapya ni pigo kwa mpango ulioanzisha na Umoja wa Mataifa hivi karibuni, kumaliza mzozo huo wa umwagaji damu uliodumu kwa miaka 3 sasa. Ijumaa iliyopita, mjumbe maalum wa umoja huo kuhusu Syria Martin Griffiths alikuwa ametangaza kwamba pande hasimu katika mzozo huo zilikuwa zimekubali kushiriki katika mazungumzo ya amani ambayo yamepangiwa kufanyika nchini Sweden mnamo siku chache zijazo.

Hapo jana, serikali ya Yemen inayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa ilithibitisha utayarifu wake kuhudhuria mazungumzo hayo, ukisisitiza lakini kwamba waasi wa kihouthi wanapaswa pia kufanya hivyo bila masharti yoyote.

Vita hivyo vilivyoanza mwaka 2015, ambavyo wachambuzi wanavichukulia kama vya 'mawakala' wa Iran na Saudi Arabia vimeuwa maelfu ya watu, na kuiharibu vibaya Yemen vikiwaweka watu wake katika hatari kubwa ya kufa kwa njaa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW