1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka mitano ya vita visivyo na mwisho Yemen

26 Machi 2020

Mzozo wa Yemen unaowapambanisha waasi wa Kihouthi na serikali hauonyeshi dalili ya kumalizika. Ikikabiliwa na vita, njaa na mapigano yasioisha, watalau wanasema ni vigumu kuirudisha nchi hiyo katika hali yake ya zamani.

Saudi Arabien Jemen Kampfjet
Picha: Getty Images/AFP/F. Nureldine

Vita vya Yemen vimeingia mwaka wake wa tano na hakuna ishara yoyote ya kuonesha vita hivyo vinaelekea mwisho. Vita hivyo kati ya wanamgambo wa Kihouthi wanaoungw amkono na Iran, na wanajeshi wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia vinaendelea huku nchi hiyo ikikabiliwa na baa la njaa.

Wataalamu wanasema hakuna ishara inayoonesha kwamba Yemen itarudi katika hali yake ya kawaida. Mwezi Machi tarehe 26 mwaka 2015 ndege za kivita za Saudi Arabia ziliingia kwenye anga ya Yemen na kuanza kushambulia ngome zote za wanamgambo  wa Kihouthi katika kile ambacho kilikuja kuwa ndio mwanzo wa mapigano makali ya kuwania udhibiti wa nchi hiyo masikini kabisa katika eneo la Mashariki ya kati.

Siku hiyo balozi wa Saudi Arabia nchini Marekani Adel al Jubeir alitangaza kwamba vikosi vya muungano vinavyoongozwa na jeshi la Saudi Arabia vitafanya kile viwezalo kuilinda serikali halali ya Yemen dhidi ya kuangushwa kutoka madarakani na dhidi ya kuangukia kwenye hatari ya aina yoyote kutoka kwa wanamgambo.

Watoto ni miongoni mwa waathirika wakubwa kabisaa wa vita vya nchini Yemen.Picha: picture-alliance/Photoshot/M. Al Wafi

''Tutafanya kila tuwezacho kuilinda serikali halali ya Yemen dhidi ya hatari yoyote. Tunakabiliwa na hali ambayo kuna kundi la wanamgambo ambalo lina uwezo wa kuwa na makombora hatari, silaha nzito nzito na kikosi cha jeshi la anga. Sikumbuki kuona katika historia kwamba kuna kundi lolote la wanamgambo lenye uwezo wa kuwa na jeshi la anga, kwa hivyo hii ni hali ya hatari sana na kwa hivyo tunabidi tufanye kila tuwezalo kuwalinda wananchi wa Yemen na serikali halali ya Yemen,'' alisema Al-Jubeir.

Kauli ya Al Jubeir ilikuwa ikiwalenga wapiganaji wa Kihouthi waliokuwa wakiushikilia mji mkuu wa Yemen Sanaa miezi michache kabla ya kuchukua kabisa madaraka ya serikali. Wakati huo kiongozi wa kundi la Houthi Mohammed al Bukhaiti alisikika akitangaza kwamba wako kwenye mchakato wa kuushinda utawala wa mabavu akimaanisha kwamba wanakaribia kukiondoa kilio cha Wahouthi dhidi ya serikali ya Yemen.

Saudi Arabia yanasa kwenye mtego

Mashambulizi ya Wahouthi yalimuondoa rais wa Yemen Abed Rabbo Mansour Hadi aliyekimbilia mjini Riyadh ambako aliomba msaada wa kijeshi wa Saudi Arabia kuilinda serikali yake siku moja kabla ya nchi hiyo ya Saudi Arabia kuanza mashambulizi mazito dhidi ya Wahouthi nchini Yemen.

Lakini sasa ni miaka mitano  na vita hivyo havikusaidia chochote zaidi ya kusababisha vifo na uharibifu. Zaidi ya watu 100,000 wameuwawa wakiwemo raia 12,000 wasiokuwa na hatia kwa mujibu wa taasisi inayofuatilia migogoro na takwimu ACLED.

Vita vya Yemen vimeongeza kile kilichoitwa na maafisa wa Umoja wa Mataifa,  janga baya kabisa la kibinadamu duniani ambapo watu wanaokadiria kufikia 85,000 walikufa kutokana na njaa iliyosababishwa na mapigano.

Mfanyakazi wa afya akiwa ndani ya kituo kipya cha karantini kilichoundwa kwa ajili ya waathirika wa virusi vya corona mjini Sanaa.Picha: Reuters/K. Abdullah

Lakini zaidi ya hayo, sasa virusi vya Corona vinavyoutikisa ulimwengu vitauporomosha kabisa mfumo wa afya wa nchi hiyo ambao tangu hapo uko taabani. Daktari mmoja wa kijerumani aliyeko Yemen, amesema kila uchao nje anasikia milio ya risasi.

Msomi mmoja kutoka taasisi inayohusika na masuala ya nchi za kiarabu za Ghuba mjini Washington anasema anahisi ni sawa sawa kusema, kwamba Saudi Arabia imenasa nchini Yemen kwa sababu ukweli wa mambo ni kwamba hawapati faida yoyote kwa kuendeleza vita hivyo lakini pia kwa upande mwingine hawawezi kuthubutu kujiondoa kwenye vita hivi.

Na juu ya hilo kile kilichokusudiwa hapo awali ni kuilinda serikali ya Hadi ili kuyalinda maslahi ya Saudi Arabia lakini hali imegeuka na kuwa kitu kingine. Na hata majaribio ya kuizuia Iran kutopata nguvu katika vita hivyo vya Yemen yamegeuka na kuwa kinyume chake.

Tokea mwanzo wa vita hivyo Wahouthi kwa kiasi kikubwa waliojiegemeza na Iran wameidhibiti sehemu kubwa ya Yemen na kuyashikilia mpaka maeneo ya karibu na mipaka ya Saudi Arabia na kuilazimu Saudi Arabia kubadili mikakati ya vita vyake.

Na kutokana na hilo wataalamu wanasema hivi sasa kipaumbele cha Saudi Arabia sio tena kurudisha uhalali nchini Yemen kama ilivyotangaza mwanzoni mwa operesheni zake bali inataka kuilinda mipaka yake upande wa kusini na kuendeleza mafungamano na makundi washirika wake ndani ya Yemen ili kupata uhakika wa maslahi yake nchini Yemen.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW