Yemen na kitisho kipya cha njaa
16 Septemba 2020Umoja wa Mataifa umezinyooshea kidole cha lawama Saudia Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Kuwait kwa kushindwa kuchangia kwa wito wa Jumuiya hiyo wa kutaka usaidizi wenye thamani ya dola bilioni 3.4 kwa ajili ya misaada ya kiutu nchini Yemen
Mark Lowcock ambaye ni mkuu wa masuala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa ameliambia Baraza la Usalama la Umoja huo kwamba katika miaka miwili iliyopita Yemen iliweza kuepuka janga la njaa kwa sababu watoa misaada walitimiza asilimia 90 ya mahitaji ya Umoja wa Mataifa na kuyawezesha mashirika ya kutoa misaada kuongeza kutoa misaada kutoka watu milioni 8 hadi milioni 12 kila mwezi. Hatua ambayo anasema ilisaidia kuokoa maisha ya mamilioni ya Wayemen.
Hata hivyo Lowcock amesema mnamo mwaka huu, Umoja huo umepokea tu asilimia 30 ambayo ni takribani dola bilioni moja kati ya wito wake wa kutaka upewe dola bilioni 3.4 kwa ajili ya mipango yake ya kibinadamu nchini Yemen, hali ambayo imesabisha takriban Wayemen milioni 9 kutopata msaada baada ya Umoja huo kupunguza misaada ya mipango hiyo ikiwemo kuwapatia chakula maji pamoja na matibabu.
Zaidi ya watu milioni 3 wameyakimbia makazi yao kutokana na mzozo wa Yemen.
Kwa mujibu wa Lowcock, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Kuwait mataifa yenye jukumu makhsusi la kutoa msaada kwa Yemen na ambalo wametimiza katika miaka ya hivi karibuni, hatahivyo mnamo mwaka huu mataifa hayo bado hayajachangia lolote kwa mipango ya Umoja huo.
Aidha ameonya kuwa ikiwa michango hiyo itaendelea kukosekana bila kutolewa kwa ajili ya misaada hilo huenda litasababisha maelfu ya Wayemen kufariki dunia kutokana na kukosa misaada ya kiutu huku akiwatolea tena wito watoa misaada kutimiza ahadi zao pamoja na kuongeza msaada wao kwa Umoja huo.
Ofisi ya Misaada ya Kiutu ya Umoja wa Mataifa, imeeleza kuwa Saudia Arabia iliaahidi kutoa dola milioni 300 kwa Umoja huo pamoja na kuahidi kutoa dola zingine 200 kwa ajili ya mipango ya kibinadamu. Umoja wa Falme za Kiarabu na Kuwait kwa upande wao hawakuahidi msaada wowote. Ofisi hiyo imeongeza.
Ikumbukwe kuwa mzozo wa Yemen umewauwa zaidi ya watu 100,000 na kusababisha janga kubwa zaidi la kibindamu duniani. Zaidi ya watu milioni 3 wamelazimika kuyakimbia makazi yao na theluthi mbili ya idadi ya Yemen hutegemea msaada wa chakula ili kuweza kuishi.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, takribani asilimia 80 au milioni 24 ya raia nchini humo wanahitaji msaada wa kiutu ama kulindwa kwa njia mmoja au nyingine.
Mashirika: AP