1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yemen wakubaliana kusitisha mapigano kwa saa 72

18 Oktoba 2016

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa pande zote nchini Yemen zimekubaliana juu mpango wa kusitisha mapigano utakaoanza Jumatano usiku. Shinikizo la kimatifa linaongezeka baada ya kushindwa kwa juhudi za awali.

Jemen Bürgerkrieg Feuerpause
Picha: picture alliance/dpa/Y. Arhab

Tangazo hilo lilikuja siku moja baada ya Marekani, Uingereza na Umoja wa Mataifa kulisihi taifa hilo kutangaza mpango mpya wa kusitisha mapigano ndani ya siku chache tu.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed, alisema amekuwa akiwasiliana na kiongozi wa ujumbe wa majadiliano wa waasi wa Kihouthi, na pia serikali ya rais wa Yemen Abdu-Rabb Mansour Hadi, inayoendesha shughuli zake kutokea mji wa kusini wa Aden.

Cheikh Ahmed alitoa taarifa Jumatatu usiku akisema amepata uhakika kutoka kwa pande zote nchini Yemen kuhusu kuanza kwa usitishaji mapigani kuanzia saa 5:59 kwa saa za Yemen siku ya Jumatano, kwa kipindi cha kuanzia cha masaa 72, kinachoweza kurefushwa.

Shambulio dhidi ya msiba Oktoba 8, 2016 liliuwa watu 140 na kusababisha ukosoaji mkubwa wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia.Picha: Getty Images/AFP/M. Huwais

"Rais amekubaliana na mpango wa usitishaji mapigano kwa masaa 72 unaoeweza kurefushwa iwapo upande wa pili utauheshimu," waziri wa mambo ya nje wa Yemen Abdulmalik al-Mekhlafi aliandika katika ukurasa wake wa twita.

Aliongeza kuwa waasi wa Kihouthi, wanaoudhibiti mji mkuu Sanaa, watahitaji pia kuamilisha kamati ya uagalizi na kukomesha mzingiro wa mji wa Taiz, wa tatu kwa ukubwa nchini Yemen.

Shinikizo lazidi kwa Saudi Arabia

Mapema Saudi Arabia - ambayo inaongoza muungano wa kijeshi kumuunga mkono Hadi - pia ilikubaliana kuhusu mpango huo mpya wa kusitisha mapigano. Wasuadi wamekabiliwa na ukosoaji mkubwa baada ya shambulio la mapema mwezi huu dhidi ya msiba ambamo watu 140 waliuawa.

Waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran wamekuwa wakitaka kumuangusha Hadi na wamechukuwa udhibiti wa sehemu kubwa ya Yemen Kaskazini na Yemen Magharibi.

Mgogoro wa Yemen umeuwa karibu watu 6,900 na kuwakosesha makaazi wengine karibu milioni tatu tangu Machi 2015 kulingana na data za Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae, DW

Mhariri:Grace Kabogo