Yemen yaonya wimbi jipya la corona
24 Februari 2021Onyo dhidi ya wimbi la pili la corona kwa Yemen limetolewa mapema leo wakati ambapo huduma za upimaji wa virusi hivyo zikiwa si za kuridhisha katika nchi hiyo iliyoharibiwa vibaya na vita.
Idadi ya visa vya COVID-19 vilivyothibitishwa imekuwa ikiongezeka katika siku 10 zilizopita baada ya ahueni ya janga hilo tangu mwezi septemba ambapo kulikuwa na visa vichache vya maambukizi kwa siku.
Visa vipya 11 viliripotiwa na kamati ya taifa ya dharura Jumatatu na Jumanne. Serikali ya Yemen imeripoti takribni visa 2,187 na vifo 620. Mamlaka za wa Houthi zinazodhibiti maeneo mengi ya mijini hayajatoa takwimu zozote kuhusu janga hilo tangu mwezi Mei walipotangaza visa vine na kifo kimoja pekee.
Ghana kupokea chanjo chini ya COVAX
Katika hatua nyingine, Ghana inatarajia kupokea awamu ya kwanza ya chanjo Covid-19 kupitia mpango wa kimataifa wa mgawanyo wa chanjo kwa nchi masikini, COVAX. Kwa mujibu wa tamko la Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, linaloratibu usafirishaji wa chanjo hizo kutoka Mumbai India likishirikiana na umoja wa mataifa, limesema kuwa linafurahi kutangaza kwamba Ghana imekuwa nchi ya kwanza kupokea chanjo hiyo. Tamko hilo linasema, dozi 600,000 za AstraZeneca ni sehemu ya chanjo zitakazosafirishwa
Ghana tayari imesharipoti visa 80,759 vya Covid-19 na vifo 582 tangu janga hilo lilipotangazwa. Watoa huduma za afya nchini humo wanatarajiwa kuwa kundi la awali litakalopata chanjo hiyo.
Wakati huohuo Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema ataipokea chanjo ya AstraZeneca huku maafisa wakihangaika kutafuta namna ya kuhakikisha kuwa dozi za chanjo hiyo ambayo haiungwi mkono na baadhi ya Wajerumani haipotei.
Kauli ya Von der Leyen imetolewa huku kukiwa na wasiwasi kuhusu maoni ya baadhi ya viongozi wa Ulaya akiwemo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ambapo kauli zao zimepunguza kasi ya kutumika kwa chanjo ya AstraZeneca, moja ya chanjo tatu pekee zilizoidhinishwa na Umoja wa Ulaya.
Mapema mwezi huu, Macron alisema kuwa Uingereza ilifanya maamuzi ya hatari kwa kuidhinisha matumizi ya chanjo ya AstraZeneca kwa pupa.