1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yuko wapi Rais Magufuli?

Jacob Safari16 Machi 2021

Leo Jumanne ni siku ya 17 tangu Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, aonekane mbele ya umma na licha uvumi ulioenea kwamba anaumwa, serikali yake bado haijatoa majibu ya wazi kuhusiana na aliko Rais huyo.

Präsident John Magufuli aus Tansania
Picha: Getty Images/AFP/M. Spatari

Yuko wapi Rais Magufuli? Ndilo swali wanalouliza wengi na swali hilo linaishia kwa watu kukamatwa na sasa wachambuzi wanasema, kimya hicho kina mshindo. Nic Cheeseman ni profesa wa demokrasia katika chuo cha Birmingham na anasema "kivyovyote vile, serikali inajaribu kupoteza muda tu na inaweza kufanya hivyo iwapo tu rais ni mgonjwa, amelemaa au amefariki" mwisho wa kunukuu.

Mara ya mwisho Magufuli kuonekana mbele ya umma ilikuwa tarehe 27 Februari na rais huyo ambaye ni muumini wa Kanisa Katoliki hajahudhuria ibada ya misa kwa Jumapili tatu sasa ambapo kama kawaida yake huwahutubia waumini wengine baadae.

Soma zaidi: Lissu asema Magufuli amehamishiwa India akiugua Covid-19

Kukosa kuonekana kwa Magufuli kunakuja wakati ambapo Tanzania imeshuhudia vifo na kile kinachoitwa "magonjwa ya kupumua" kuyakumba majina makubwa ya kisiasa nchini humo. Ila wiki moja kabla kuonekana kwake, rais huyo wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki alikiri kwamba virusi vya corona, vinasambaa nchini mwake hasa baada ya kifo cha makamu wa rais wa Zanzibar, Maalim Seif ambaye baadae iliripotiwa kwamba amefariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Upinzani wamtaka spika aweke wazi taarifa kuhusiana na afya ya Rais

Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Zitto KabwePicha: DW/E. Boniphace

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO barani Afrika, Dokta Matshidiso Moeti, amesema shirika hilo lingependa Tanzania ijiunge na nchi zengine duniani katika juhudi za utoaji chanjo ikiwemo kujiunga na mpango wa COVAX unaotoa chanjo kwa nchi maskini duniani, ili iwakinge raia wake kutokana na kuenea kwa virusi vya corona.

"Nafikiri kwa hali yoyote ile aliyo Rais Magufuli, tunaweza tu kumtakia kila la heri iwapo haya yanayosemwa ni kweli na tunautangaza tena msimamo wetu wa kuwa tayari kuisaidia serikali ya Tanzania na watu wake."

Jumanne iliyopita, kiongozi wa upinzani ambaye anaishi Ubelgiji, Tundu Lissu, alianza kuuliza maswali kuhusiana na uwepo wa rais huyo akisema kwamba duru zimemuarifu kwamba anaugua na magonjwa mengine ya awali aliyokuwa nayo yamesababisha hali yake kuwa mbaya zaidi.

Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe amesema kuwa katiba ya Tanzania inamtaka spika wa bunge kuweka wazi taarifa kuhusiana na afya ya rais, akisema haifai kuwa siri kwani Watanzania walikuwa wakipokea taarifa kuhusu afya za marais wao wa zamani Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete walipokuwa nje ya nchi wakipokea matibabu.

Shirika la habari la Reuters limejaribu kumtafuta msemaji wa serikali Hassan Abbasi atoe tamko kuhusiana na suala hilo la afya ya rais Magufuli ila hajajibu simu wala ujumbe waliomtumia.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW