Zahma ya mabomu ya jumuia ya NATO mjini Tripoli
8 Juni 2011Muammar Gaddafi anasema hatosalimu amri licha ya hujuma za madege ya jumuia ya kujihami ya NATO kugharimu maisha ya watu 31, na rais Barack Obama wa Marekani akisema hujuma hizo zitaendelea mpaka kiongozi huyo wa Libya anang'oka madarakani.
Hujuma hizo zinazosemekana kuwa kali kupita zote tangu jumuia ya kujihami ya NATO ilipoanza kuushambulia mji mkuu wa Tripoli zimefanyika mnamo siku ya kuzaliwa Muammar Gaddafi. Msemaji wa serikali ya Libya, Mussa Ibrahim, amesema NATO imevurumisha mabomu 60 na kuwauwa raia 31 na dazeni kadhaa kujeruhiwa .
Msemaji wa jumuia ya kujihami ya NATO, Mike Bracken amesema kwa upande wake "wataendelea kuukaba utawala wa Libya na kuzuwia nguvu zake za kutoa amri kupitia vituo vya uongozi wa kijeshi.
Mjini Washington, rais Barack Obama alikuwa mkali zaidi aliposema "Gaddafi anabidi aondoke madarakani na kuwakabidhi madaraka wananchi wa Libya na kwamba shinikizo litazidi hadi atakapong'atuka."
Waziri wake wa mambo ya nchi za nje, bibi Hillary Clinton, ameelekea Abu Dhabi hii leo kushauriana na nchi zinazounga mkono opereshini za kijeshi dhidi ya Libya, na kusaka njia za kuzidi kuusaidia upande wa upinzani nchini humo.
Na mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa nchini Libya, Abdel Ilah al Khatib wa Jordan, amewasili Benghazi hii leo kwa mazungumzo pamoja na wanachama wa baraza la taifa la mpito-linaloongozwa na upande wa upinzani.
Bwana Khatib ametokea Tripoli ambako msemaji wa serikali, Moussa Ibrahim, amesema "alikuwa na mazungumzo ya maana pamoja na maafisa wa serikali ya Libya."
Jana mjumbe maalum wa rais wa Urussi, Dmitri Medvedev, Mikhael Marguelov, alikuwa pia ziarani Benghazi. Amezungumzia nia ya serikali ya Moscow ya kutaka kurahisisha mazungumzo kati ya serikali ya kanali Gaddafi na waasi. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Serguei Lavrov, amesema hata hivyo, nchi yake haitaki kujibebesha jukumu la upatanishi, akisisitiza hilo ni jukumu la Umoja wa Afrika.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp
Mhariri:Miraji Othman