Zaidi ya raia 130 wauawa na waasi wa M23 yasema ripoti ya UN
8 Desemba 2022Uchunguzi huo wa awali uliendeshwa kwa pamoja na ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa MONUSCO na Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya umoja huo. Taarifa ya pamoja ya ujumbe huo imesema mauaji ya Novemba 29 na 30 katika vijiji vya Kishishe na Bambo yalifanywa kama sehemu ya kulipiza kisasi mapigano kati ya kundi la M23 na makundi pinzani yenye silaha.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema Waathiriwa waliuawa kiholela kwa risasi au kwa mapanga.Wachunguzi waliwahoji waathiriwa na mashahidi wa moja kwa moja 52 pamoja na vyanzo vingine mbalimbali katika eneo la Rwindi, kama kilomita Ishirini kutoka Kishishe, ambako manusura na mashahidi walikuwa wamekwenda kujificha.
''Waliwakata vichwa''
Muhindo Mukambati ameiambia DW kwamba mdogo yake wa miaka 20 na wavulana wengine wanane waliuliwa kwa kukatwa vichwa.
''Ilikuwa katika kijiji cha Kishishe na walikuwa watu tisa. Walikuwa miongoni mwa vijana ambao waliwabebea mizigo ya vitu walivyopora katika makaazi na maduka ya raia. Walipofika msituni waliwakata vichwa na kuacha mili zao huko.'', alisema Muhindo.
Uchunguzi wa kimataifa ?
Umoja wa Mataifa unalaani kwa maneno makali zaidi unyanyasaji dhidi ya raia na kutoa wito wa ufikiaji usio na kikomo eneo la tukio na waathiriwa kwa msaada wa dharura wa kibinadamu.
Jumatatu, serikali ya Kongo ilishutumu kundi la M23 kwa kuua watu 272. Na kutangaza kuwa imewasilisha ombi la kueko na uchunguzi wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC.
M23 yakanusha mauwaji ya raia
Wanamgambo hao wa M23 ambao wameteka miji kadhaa karibu na mipaka ya Rwanda na Uganda mwaka huu, wamekanusha kuhusika na mauwaji hayo na kuomba uchunguzi kamili. Msemaji wa kundi hilo, Lawrance Kanyuka ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa Umoja wa Mataifa uko chini ya shinikizo kutoka kwa serikali kutoa takwimu, hata kama ni za uongo.
Mashambulizi ya hivi majuzi ya waasi wa M23 yamesababisha maelfu ya raia kuyahama makaazi yao na kuzua mzozo wa kidiplomasia na nchi jirani ya Rwanda. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanashutumu Rwanda kuunga mkono wanamgambo, huku Kigali ikiwa ikikanusha shutuma hizo.