1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya raia elfu kumi wazuiliwa kuondoka Sievierodonetsk

Saleh Mwanamilongo
9 Juni 2022

Mapigano yanaendelea kupamba moto katika mitaa ya Sievierodonetsk mashariki mwa Ukraine. Huku zaidi ya raia elfu kumi wakizuiliwa katika mji huo.

Mashambulizi makali Sievierodonetsk
Mashambulizi makali SievierodonetskPicha: Ukrainian State Emergency Service/AFP

Gavana wa jimbo la Mashariki la Luhansk, Serhiy Haidai,amesema Urusi inashambulia kwa makombora maeneo ya jiji la Sievierodonetsk,ambayo bado yanadhibitiwa na Ukraine. Anasema vikosi vya Ukraine vingeweza kujihami endapo vingekuwa na silaha za masafa marefu.

''Hospitali zote katika eneo la mkoa wa Luhansk, ambazo ziko chini ya udhibiti wa Ukraine, zote zimeshambuliwa kwa makombora. Kila kitu kuhusu miundombinu muhimu - gesi, maji, umeme,hushambuliwa kwa makusudi. Halafu, hata vituo vya dharura au hospitali, ambazo ziko sasa kwenye eneo jipya linalokaliwa, wanapora vifaa huko. Wakazi wanaona yote kwa uwazi. Ikiwa nyinyi ni 'wakombozi' kama hao, kwa nini basi mnapora vifaa kutoka kwa wenyeji?" alisema Haidai.

Hii leo, Meya wa mji wa Sievierodonetsk, Oleksendr Stryuk amesema vikosi vya Ukraine bado vinashikilia eneo la viwanda katika jiji hilo. Anasema hali ni "ngumu lakini inaweza kudhibitiwa. Stryuk amesema safu za ulinzi zilikuwa zikishikilia licha ya mashambulizi makali ya vikosi vya Urusi, na kwa sasa ni vigumu kuwaondoa raia kutoka Sievierodonetsk. Alisema takriban raia 10,000 walibaki ndani mji, ambao sasa ni lengo kuu la mashambulizi ya Urusi.

Zaidi ya raia 10,000 walibaki ndani mji wa Sievierodonetsk Picha: Mykola Berdnyk/DW

Urusi inakanusha kuwalenga raia na imepinga tuhuma za uhalifu wa kivita. Shirika la habari la Urusi, RIA, limeripoti kuwa Waingereza wawili na Mmorocco ambao walitekwa wakati wakiunga mkono jeshi la Ukraine wanaweza kukabiliwa na hukumu ya kifo baada ya kukiri kuwa na hatia.

Kwa upande wake rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema mamilioni ya watu wanaweza kufa njaa kwa sababu ya kuzuwiliwa kwa bandari za Bahari Nyeusi na Urusi. Zelenskiy amesema dunia iko ukingoni mwa mgogoro mbaya wa chakula, na Ukraine haiwezi kuuza nje kiasi kikubwa cha ngano, mahindi, mafuta na bidhaa nyingine ambazo zilikuwa zikileta utulivu katika soko la kimataifa. Urusi imeteka sehemu kubwa za pwani ya Ukraine karibu Wiki 15 za vita na meli zake za kivita zinadhibiti Bahari Nyeusi ya Azov.

Akitarajia kufanya ziara mji Kyiv hii leo, waziri wa Afya wa Ujerumani Karl Lauterbach anapanga kutoa huduma ya matibabu kwa wapiganaji wa Ukraine waliojeruhiwa kwenye mapigano.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW