Zaidi ya nusu ya watu wa Sudan wanahitaji msaada
15 Novemba 2025
Katibu Mkuu wa Baraza la Wakimbizi la Denmark Charlotte Slente ameliambia wiki hii shirika la habari la AFP baada ya ziara yake katika eneo la mpakani mwa Chad na Sudan na kusema alishuhudia hali ambayo zaidi ya watu milioni 30 wanahitaji msaada wa kibinadamu, hiyo ikiwa ni nusu ya idadi jumla ya watu wa Sudan na kusisitiza kuwa "mateso aliyoyashuhudia hayafikiriki."
Vita hivyo vilivyoanza mnamo Aprili mwaka 2023, kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha RSF vimewaua makumi ya maelfu ya watu, kuwalazimisha wengine karibu milioni 12 kuyahama makazi yao na hivyo kusababisha moja ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani.
Mwaka 2024, Sudan ilikuwa na idadi ya watu wapatao milioni 50, hii ikiwa ni kulingana na Benki ya Dunia. Kauli ya Afisa huyo wa shirika la misaada imetolewa siku chache baada ya kulitembelea eneo moja nchini Chad linalopakana na Darfur huko magharibi mwa Sudan, ambako kumeshuhudiwa mapigano makali katika siku za hivi karibuni.
Vurugu zaongezeka Darfur
Vurugu zimeongezeka kwa kasi katika wiki za hivi karibuni, huku wanamgambo wa RSF wakichukua udhibiti wa mji muhimu wa El-Fasher baada ya kuuzingira kwa miezi 18 huku ripoti za ukatili zikifichuliwa. Mji huo wa El-Fasher ndio ulikuwa ngome ya mwisho ya jeshi la Sudan huko Darfur.
"Maeneo hayo, kuna vitendo vinavyokiuka sheria zote za kimataifa za kibinadamu," aliongeza Bi Slente na kusisitiza pia kuwa shirika hilo lisilo la kiserikali limeshuhudia vitendo vya mauaji ya halaiki na unyanyasaji wa kingono nchini Sudan.
"Tumeshuhudia ukamataji kiholela, utekaji nyara, kuwalazimisha raia kuyahama makazi yao pamoja na mateso mbalimbali, " alielezea afisa huyo huku akiishutumu jumuiya ya kimataifa kwa kutochukua hatua za kutosha ili kuishughulikia hali hiyo.
"Ripoti hazisaidii kurekebisha hali"
Katibu huyo Mkuu wa Baraza la Wakimbizi la Denmark Charlotte Slente amesema taarifa zinazotolewa zina athari ndogo mno ukilinganisha na mahitaji ya kibinadamu yanayoshuhudiwa nchini Sudan, na kwamba licha ya kuwa ripoti zinaendelea kutolewa, hazijaweza kuzuia vurugu..
Bi Slente ametahadharisha kwamba kulikuwa na miji mingine huko Sudan ambayo bado imezingirwa na ambayo haikuwa ikipokea kiwango sawa cha kuangaziwa na kushughulikiwa. Aliutaja miji wa Babanusa, ngome ya mwisho ya jeshi katika jimbo la Kordofan Magharibi, ambao umekuwa ukizingirwa kwa miezi kadhaa, pamoja na mji mkuu wa jimbo la Kordofan Kaskazini wa El-Obeid na miji ya Kadugli na Dilling huko Kordofan Kusini.
"Jumuiya ya kimataifa lazima iache kudhibiti matokeo ya mzozo huu na lazima ianze kuzuia vitendo vya ukatili," alisema Slente.
//AFP