1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya nusu ya watoto wakimbizi hawaendi skuli

29 Agosti 2018

Zaidi ya nusu ya watoto wakimbizi wenye umri wa kwenda skuli hawana fursa ya kupata elimu, huku mataifa ulimwenguni yakikabiliana na ongezeko kubwa la wakimbizi katika historia ya hivi karibuni.

Türkei Flüchtlinge aus Syrien
Picha: picture-alliance/AP Photo/L. Pitarakis

Watoto milioni nne wakimbizi duniani hawaendi skuli, likiwa ni ongezeko la watoto nusu milioni ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka mmoja tu uliopita, inasema ripoti ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR).

Mkuu wa shirika hilo, Filippo Grandi, alisema siku ya Jumatano (29 Agosti) kwamba licha ya elimu kuwa njia ya kuwaponya watoto hao na pia ya kuzifufua nchi zilizokumbwa na majanga yaliyosababisha wakimbizi, hali inazidi kutisha kwa watoto hao.

"Kutokana na hali ilivyo sasa, endapo uwekezaji wa dharura haukufanyika, basi maelfu ya watoto watajikuta kuwa sehemu ya takwimu hizi za kuogofya," alisema mkuu huyo wa UNHCR.

Kufikia mwishoni mwa mwaka uliopita, shirika hilo lilikuwa linawahudumia zaidi ya wakimbizi milioni 20, huku milioni 7.4 wakiwa watoto wenye umri wa kwenda skuli - idadi ambayo haijumuishi wengine wapatao milioni 5 kutoka Palestina - lakini ni asilimia 61 tu ya watoto wakimbizi walioweza kusoma elimu ya msingi, ikilinganishwa na asilimia 90 ya watoto wasiokuwa wakimbizi, kwa mujibu wa ripoti hiyo. 

Hali mbaya zaidi kwa wasichana na wavulana wa umri mkubwa

Mjengeko wa kijamii na kitamaduni unawaweka watoto wa kike kwenye nafasi ngumu zaidi kupata elimu wawapo kwenye makambi ya wakimbizi.Picha: Reuters/J. Akena

Licha ya kwamba watoto zaidi ya 500,000 waliandikishwa kuanza masomo mwaka jana, lakini kwa kuwa idadi ya wakimbizi inazidi kuongezeka kila uchao, idadi hiyo ni ndogo sana kulinganisha na uhalisia.

Mshauri wa masuala ya elimu kwenye shirika la misaada ya kiutu la Marekani, Care USA, Katherine Begley, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba hata ile fursa ndogo ya kupata elimu waliyonayo watoto wakimbizi nayo inakumbwa na changamoto nyingi, ikiwemo miundombinu mibovu na ukosefu wa vifaa vya kujifunzia.

Hali ni mbaya zaidi kwa watoto wenye umri mkubwa, ambapo ni mmoja tu katika kila wanne ndiye aliyeweza kupata elimu ya sekondari. Kwenye sekondari ya juu ni asilimia moja tu ya watoto wakimbizi waliomudu, ilhali kwa watoto wasiokuwa wakimbizi ni zaidi ya robo tatu.

Kwa mujibu wa Fransisca Vigaud-Walsh, mtafiti mwandamizi wa haki za wanawake na wasichana, "watoto wa kike wakimbizi ndio walio kwenye hatari ya kukosa elimu kutokana na mjengeko wa kijamii na kitamaduni kwa familia za wakimbizi."

Matokeo ya hilo, ni pamoja na ndoa za kulazimishwa, ufanyishwaji kazi kwa kulazimishwa na hata biashara haramu ya binaadamu dhidi ya watoto wa kike wakimbizi.

Ili kukabiliana na tatizo hilo, shirika la UNCHR linasema watoto wakimbizi wanapaswa sasa kuandikishwa kwenye skuli za kawaida kuliko kwenye skuli zao maalum, wapatiwe msaada wa ziada, na vikwazo kama vile mahitaji ya nyaraka rasmi za kusajiliwa, lazima viondoshwe.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW