1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya waasi 150 wa Yemen wauawa katika mashambulizi Yemen

15 Oktoba 2021

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen ambao unaiunga mkono serikali, umesema kuwa zaidi ya waasi 150 wa Kihouthi wameuawa katika mashambulizi ya anga yaliyofanyika jana kwenye jimbo la Marib.

Jemen | Kämpfe in Marib
Picha: AFPTV/AFP/Getty Images

Taarifa hiyo iliyotangazwa kupitia shirika la habari la Saudi Arabia imeeleza kuwa mashambulizi ya anga ya hivi karibuni dhidi ya waasi hao wanaoungwa mkono na Iran yamesababisha mauaji hayo yaliyotokea katika wilaya ya Abdiya iliyopo kwenye jimbo hilo lenye utajiri wa mafuta.

Muungano huo umesema zaidi ya waasi 500 wameuawa ndani ya kipindi cha siku nne na katika mashambulizi hayo ya jana, magari 11 ya kivita yameharibiwa. Muungano huo ulifanya mashambulizi 36 ya anga katika kipindi cha saa 24.

Waasi waanzisha mashambulizi

Waasi wa Kihouthi walianzisha tena kampeni yao ya kulitwaa jimbo la Marib, ngome muhimu ya mwisho ya serikali. Waasi hao huzungumza kwa nadra kuhusu hasara na maafa ya kivita wanayopata, hivyo idadi hiyo ya vifo haikuweza kuthibitishwa na shirika la habari la AFP.

Katika taarifa yao waliyoitoa siku ya Jumanne, waasi hao walisema wako ukingoni kuuchukua mji huo. Kwa mujibu wa mmoja wa maafisa, licha ya kupoteza wapiganaji wao, waasi wa Kihouthi wanazidi kusonga mbele. Duru za jeshi linaloiunga mkono serikali, zimesema wapiganaji wake 23 wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika kipindi cha saa 48 zilizopita.

Wapiganaji wa Yemen wanaoungwa mkono na Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia huko MaribPicha: Nariman El-Mofty/AP Photo/picture alliance

Ama kwa upande mwingine mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Hans Grundberg amesema pengo kati ya pande zinazohasimiana nchini Yemen ni kubwa na linaongezeka. Kauli hiyo ameitoa kufuatia mikutano aliyoifanya na serikali ya Yemen mjini Riyadh na Aden pamoja na Ansar Allah, mjini Muscat.

''Maoni yangu ambayo nimewashirikisha ni kwamba wakati mchakato wa muda unapaswa kuwa wa dharura kuhusu masuala ya kibinaadamu na kiuchumi, suluhisho la kudumu linaweza kupatikana tu kupitia suluhu kamili ya mazungumzo ya kisiasa,'' alisema Grundberg.

Maelfu hawana makaazi

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamiaji, IOM, limesema maelfu ya watu hawana makaazi kutokana na mapigano yanayoendelea kwenye jimbo la Marib kwa mwaka huu, huku takwimu zikipanda kutokana na mapigano yaliyoongezeka mwezi uliopita. IOM imesema kuanzia Januari Mosi hadi Septemba 30, imerekodi zaidi ya watu 55,000 ambao wameyakimbia makaazi yao kwenye jimbo la Marib.

IOM imefafanua kuwa takribani watu 10,000 waliyakimbia makaazi yao mwezi uliopita pekee, hiyo ikiwa idadi kubwa kushuhudiwa kwenye jimbo hilo kwa mwaka huu. Kabla ya kuanza kwa vita, jimbo hilo lilikuwa na kati ya wakaazi 20,000 hadi 30,000. Lakini idadi hiyo iliongezeka kwa maelfu ya watu kutokana na utulivu wake, wakati ambapo raia wa Yemen walipoyakimbia maeneo yaliyokumbwa na mapigano.

Nayo Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kiutu, OCHA, imesema miundombinu muhimu kama vile madaraja na barabara vimeharibiwa vibaya na mashambulizi.

(AFP, AP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW