1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya wanajeshi 80 wauwawa Yemen

19 Januari 2020

Waasi wa Houthi wawashambulia wanajeshi wa serikali wanaosaidiwa na kikosi cha muungano, kwenye mkoa wa Marib na kuwauwa zaidi ya 80 na kuwajeruhi wengine wengi

Jemen Anschlag auf Polizeikräfte in Aden
Picha: Reuters/F. Salman

Zaidi ya wanajeshi 80 wa Yemen wameuwawa na wengine wengi walijeruhiwa kwenye shambulizi la kombora na ndege zisizokuwa na rubani yaliyofanywa na waasi wa Houthi katikati ya Yemen.Vyanzo vya taarifa hii ni maafisa wa afya na jeshi.

Mashambulizi hayo yamefanyika Jumamosi na yanafuatia miezi kadhaa ya utulivu kiasi katika nchi hiyo inayokabiliwa na vita kati ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran na serikali inayotambuliwa kimataifa na ambayo inasaidiwa kwenye vita hivyo na jeshi la muungano linaloongozwa na Saudi Arabia.

Picha: Getty Images/AFP/A. Al-Quadry

Waasi wa Houthi walishambulia msikiti mmoja katika kambi ya kijeshi iliyoko kwenye mkoa wa kati wa Marib kiasi kilomita 170 Mashariki mwa mji mkuu Sanaa wakati wa sala ya Magharibi,kwa mujibu wa vyanzo vya kijeshi vilivyozungumza na shirika la habari la AFP.

Chanzo kutoka hospitali ya mjini Marib ambako wahanga wengi waliojeruhiwa walipelekwa kimesema wanajeshi 83 waliuwawa na 148 walijeruhiwa kwenye shambulio hilo. Mara kwa mara suala la  idadi ya wanaouwawa katika mgogoro wa Yemen ni linazusha ubishi nchini humo lakini idadi hii kubwa ya wanajeshi waliouwawa Marib inaonesha kuwa ni moja ya shambulio baya kabisa lililosababisha umwagikaji mkubwa wa damu kwa wakati mmoja tangu vita hivyo vilipoanza mwaka 2014,waasi wa Kihouthi walipoudhibiti mji mkuu Sanaa.

Mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani na makombora yamefanyika siku moja baada ya wanajeshi wa serikali wanaoungwa mkono na  kikosi cha muungano kuanzisha operesheni kubwa dhidi ya Wahouthi katika mkoa wa Nihm Kaskazini mwa Sanaa. Mapigano kwenye eneo hilo la Nihm yanaendelea leo, Jumapili kwa mujibu wa duru ya kijeshi, na waasi kadhaa wameuwawa na wengine kujeruhiwa duru hiyo imeeleza.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Lilian Mtono

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW