Zaidi ya Wapalestina 130, Waisraeli 9 wauawa
15 Mei 2021Siku ya Jumamosi (Mei 15), madaktari katika Ukanda wa Gaza walisema watu saba walikuwa wameuawa kufuatia mashambulizi ya anga ya jeshi la Israel katika eneo la kaskazini la Ukanda huo.
Wakaazi wa huko waliripoti pia taarifa za jeshi la wanamaji la Israel kurusha makombora kutokea Bahari ya Mediterenia.
Katika mitaa ya Ukingo wa Magharibi, wanajeshi wa Israel waliwauwa waandamanaji saba wa Kipalestina siku ya Ijumaa (Mei 14), wakati ghasia zikizuka katika maeneo mbalimbali ya Israel, ambako raia wa Kiyahudi na Kiarabu wanapambana.
Milio ya ving'ora vya tahadhari ilisikika kwenye miji mikubwa miwili ya kusini mwa Israel asubuhi ya Jumamosi, baada ya Hamas kurusha makombora mengine kutokea Gaza.
Tangu mapigano kuanza siku ya Jumatatu, zaidi ya makombora 2,000 yamesharushwa kutokea Gaza kuelekea Israel, yakiwauwa watu tisa, mmoja mtoto mdogo na mwanajeshi mmoja na kujeruhi watu 560.
Juhudi za upatanishi
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitazamiwa kukutana siku ya Jumapili (Mei 16) kujadili mapigano yanayoendelea kati ya Israel na kundi la Hamas.
Waziri anayeshughulikia masuala ya Palestina na Israel kwenye serikali ya Marekani, Hady Amr, aliwasili nchini Israel siku ya Ijumaa kama sehemu ya juhudi za kupatanisha.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Jalina Porter, alisema Amr angelifanya mazungumzo na maafisa wa Israel na Palestina walioko Ukingo wa Magharibi, kusisitiza kusitishwa kwa mapigano.
Kawaida, Marekani huwa haizungumzi na Hamas, inayosema ni kundi la kigaidi.
Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye anatuhumiwa kuvitumia vita hivi kujiokowa kisiasa, hakuwa ameonesha ishara yoyote ya kulegeza kampeni yake ya kijeshi dhidi ya Gaza.
Hadi sasa, Israel inasema imeshapiga maeneo takribani 800 ndani ya Ukanda wa Gaza, ikiwemo njia ya chini kwa chini inayotumiwa na wanamgambo wa Hamas.
Kufikia asubuhi ya Jumamosi, Israel ilikuwa inakisia kuwa ilishafanikiwa kuwauwa zaidi ya makamanda 30 Kipalestina kwa mashambulizi yake.
Umoja wa Mataifa ulisema wakaazi wapatao 10,000 wa Gaza wamelazimika kuyakimbia makaazi yao.