Zaidi ya watu 20 wauwawa Gaza katika mashambulizi ya Israel
11 Desemba 2024Msemaji wa shirika la ulinzi wa raia la Gaza Mahmud Bassal amesema mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel usiku kucha yamesabaisha vifo vya zaidi ya watu 20, ambapo yaliilenga nyumba ya familia ya Abu al-Tarabish karibu na hospitali ya Kamal Adwan. Bassal, amesema katika mashambulizi hayo, ndege ya kivita ya Israel ilirusha makombora matatu usiku wa manane.
Kulingana na kumbukumbu za hospitali ya Kamal Adwan miongoni mwa watu waliouawa ni wanafamilia sita. Taarifa ya hospitali hiyo imesema, shambulio jingine liliilenga kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati mwa Gaza, ambako watu saba wameuawa. Kati ya waliouwawa ni watoto wawili, wazazi wao na ndugu wengine watatu.
Nalo jeshi la Israel limesema wanamgambo wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza wamerusha makombora manne kuelekea Israel mapema Jumatano. Aidha jeshi hilo limesema makombora mawili yalizuiwa wakati mawili yaliyosalia yaliangukia katika eneo la wazi ambalo halina makazi ya watu.
Wapalestina wanazidi kukabiliwa na hali mbaya ya kiutu
Mzozo kati ya Israel na Hamas, hadi sasa umesababisha kuuwawa kwa zaidi ya Wapalestina 44,000 kwa mujibu wa takwimu za mamlaka za Afya za Palestina zilizo chini ya kundi la Hamas. Ni wakati Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya Kiutu OCHA ikisema kuwa misaada ya kiutu inayopaswa kuingia katika Ukanda wa Gaza imezuiwa kwa kiasi kikubwa katika siku 66 zilizopita.
Hali hiyo imesababisha Wapalestina kati ya 65,000 na 75,000 kukosa huduma za chakula, maji, umeme au huduma za afya. Mratibu mwandamizi wa uratibu wa misaada ya kibinadamu wa Ofisi hiyo kwa Gaza Sigrid Kaag amesema licha ya kuwa na matumaini ya vita kusitishwa, hali ni ngumu.
Ameeleza kuwa, "Tumezungumzia matumaini yetu juu ya vita kusitishwa na kuachiliwa kwa mateka bila masharti yoyote, na hili litawezesha ongezeko la misaada. Lakini hatimaye nimeona hali ngumu huku wakazi wa Gaza wakiendelea kuteseka."
Kwa mujibu wa Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya Kiutu Wapalestina katika maeneo ya Beit Lahiya, Beit Hanoun, na Jabaliya ambayo yamezingirwa na majeshi ya Israel kwa kiasi kikubwa wanakoseshwa misaada na wanaishi katika mazingira magumu ya kutisha.