1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Zaidi ya watu 2,000 walifariki kwenye eneo la Karamoja

23 Mei 2023

Ripoti mpya ya tume ya haki za binadamau nchini Uganda, imefichua kuwa zaidi ya watu 2,000 walipoteza maisha mnamo mwaka 2022 kwenye eneo la Karamoja kaskazini mwa Uganda.

Klimakrieg in Karamoja Timothy Stammesführer
Picha: Simone Schlindwein

Ripoti hiyo imeelezea kipindi kirefu cha kiangazi, kuzorota kwa usalama na utapiamlo kuwa vyanzo vya baa la njaa na vifo kwenye eneo hilo.

Soma pia: Waziri mwingine Uganda apelekwa rumande kwa wizi wa mabati

Kwa mujibu wa ripoti hiyo watu 2, 207 walipoteza maisha yao kutokana na njaa mwaka huo hasa mwezi Julai. Habari hizo zimeibua hisia mseto za huzuni na ghadhabu miongoni mwa wananchi wakihoji vipi idadi kubwa kama hiyo ya raia wanaweza kufariki kutokana na uhaba wa chakula huku serikali ikiwapangia tu kupata mabati ya kuezeka nyumba ambayo pia kuda madai kwamba yaliibwa na mawaziri. Geofrey Ekisa ni mmoja kati ya watu waliojitolea kusaidia kukusanya chakula kutoka mji wa kampala kutoka kwa watu wenye mapenzi mema na kuwapelekea watu wa eneo hilo.

Soma pia: Serikali ya Uganda yatakiwa kuimarisha usalama Karamoja

Jitihada zilizopo

Picha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Ripoti hiyo inaelezea kuwa juhudi za watu wa Karamoja kujaribu kukumbatia kilimo ili kuacha kutegemea misaada ya chakula zinatambuliwa. Ila mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuzorota kwa usalama vimekwaza jitihada hizo pamoja na kwamba hawajapata ushauri stahiki kuhusu njia zipi bora za kilimo wanazofaa kuzingatia. Kulingana na ripoti hiyo, watu 1,676 walifariki katika wilaya ya Kotido iliyo kwenye makutano ya Uganda na mataifa jirani ya Sudan Kusini, Kenya na Ethiopia. Watu hao idadi kubwa wakiwa walifariki baada ya kukumbwa na utapiamlo.

Soma pia: Watu 200 wauawa eneo la Karamoja tangu mwaka huu uanze

Kijadi, jamii ya Karamoja ni wafugaji wa kuhamahama na kufuatia kushamiri kwa wizi wa mifugo uliochochewa na kuzorota kwa usalama, wengi walipoteza mifugo yao na kuishi maisha ya utegemezi kwa misaada ya chakula. Wanaume wengi walikata tamaa na maisha na kugeukia ulevi wa kupindukia. Ni kwa ajili hii ndiyo ripoti hiyo ya tume ya haki za binadamu ya Uganda inapendekeza serikali ijitokeze na mikakati ya kutatua changamoto zote kwa pamoja. Si ajabu kwamba idadi kubwa ya watoto wa mitaani kwenye miji ya Uganda ni wale kutoka sehemu hiyo ya karamoja. Wao hushuhudiwa wakiombaomba kwenye misongamano ya magari katika mji wa kampala na kwingineko. 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW