1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 30 wauawa Afghanistan

15 Oktoba 2021

Takribani watu 32 wameuawa katika shambulizi lililotokea kwenye msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Kishia kusini mwa Afghanistan.

Afghanistan l Bombenexplosion in einer Moschee in Kandahar
Picha: Murteza Khaliqi/AA/picture alliance

Afisa wa afya wa jimbo la Kandahar, Musa Jan Sultani amesema watu wengine zaidi ya 70 wamejeruhiwa katika shambulizi hilo lililotokea Ijumaa mchana. Mtu aliyeshuhudia amesema alisikia miripuko mitatu, ambapo moja limetokea kwenye lango kuu la msikiti, jingine upande wa kusini na la tatu ambako waumini walikuwa wakinawa kabla ya kuanza swala.

Wiki moja baada ya shambulizi la Kunduz 

Shambulizi la Ijumaa linatokea wiki moja baada ya shambulizi jengine la kujitoa muhanga kwenye mji wa Kunduz kuwaua zaidi ya waumini 40 wa Kishia katika msikiti. Kundi la wanamgambo linalofungamana na linalojiita Dola la Kiislamu, IS-K kwenye jimbo la Nangarhar, lilikiri kuhusika na shambulizi hilo la Kunduz.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya serikali ya Taliban, Qari Sayed Khosti, amesema wamesikitishwa na shambulizi hilo ambalo limesababisha mauaji ya waumini hao wa Kishia na kuwajeruhi wengine. Khosti amesema vikosi maalum vya Emarati ya Kiislamu ya Afghanistan vimewasili kwenye eneo la tukio kubaini chanzo cha shambulizi hilo na kuwafikisha wahalifu katika vyombo vya sheria.

Majeruhi wa shambulizi la Kunduz wiki iliyopita akipakizwa kwenye gari la wagonjwaPicha: Abdullah Sahil/AP Photo/picture alliance

Ukurasa wa Facebook wa msikiti huo umetoa ombi la watu kuchangia damu. Serikali mpya ya Taliban ambayo imechukua madaraka Afghanistan katikati mwa mwezi Agosti baada ya kuondoka kwa majeshi ya Marekani, imeapa kurejesha utulivu nchini humo na kuwalinda waumini wa Kishia ambao ni wachache.

Asilimia 20 ni Washia

Washia ni asilimia 20 ya idadi ya Waafghani, huku wengi wao wakiwa wa jamii ya Hazara, kabila dogo ambalo limekuwa likiteswa kwa miongo kadhaa nchini Afghanistan.

Wakati huo huo, Rais wa Urusi, Vladmir Putin amesema kundi la Taliban limekubali kushiriki katika mazungumzo kuhusu Afghanistan yatakayofanyika wiki ijayo. Akizungumza kwa njia ya video na viongozi wa mataifa mengine yaliyokuwa kwenye Muungano wa Kisovieti, hata hivyo, Rais Putin amesema hakuna haja ya kuharakisha kuutambua rasmi utawala wa Taliban, ingawa kuna haja ya kufanya nao mazungumzo.

Rais wa Urusi, Vladmir PutinPicha: Ramil Sitdikov/SNA/imago images

''Tunaelewa kwamba tunapaswa kushirikiana na Taliban, lakini hatuna ulazima wa kuharakisha kuwatambua. Tutajadiliana kuhusu hili na kufanya mashauriano pamoja. Hata hivyo, tunapaswa kudumisha mchakato wa maridhiano ya Afghanistan na kuifanya hali kuwa ya kawaida kwenye nchi hii,'' alifafanua Putin.

Ahadi ya kuitisha uchaguzi

Putin amesema serikali ya mpito iliyoanzishwa na Taliban kwa bahati mbaya haiakisi jamii yote ya Afghanistan, lakini amegusia pia ahadi yao ya kuitisha uchaguzi na juhudi zao za kurejesha utendaji wa taasisi za serikali.

Aidha, Putin amezungumzia nia yake ya kuitisha duru nyingine ya mazungumzo kati ya pande za Afghanistan wiki ijayo. Amesisitiza kuna umuhimu wa kuanza upya mazungumzo ya Afghanistan kati ya Urusi, Marekani, China na Pakistan, ili kuunga mkono mchakato wa makaazi kwa ajili ya Waafghani na kujaribu kusaidia kurekebisha hali nchini humo.

     

(AFP, DPA, AP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW