1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaChina

Watu zaidi ya 90 wafariki kufuatia tetemeko la ardhi Tibet

7 Januari 2025

Watu zaidi ya 90 wamekufa na wengine kadhaa wamejeruhiwa kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililotokea karibu na moja ya miji mitakatifu zaidi ya eneo la China lenye mamlaka ya ndani la Tibet.

Uharibifu kutokana na tetemeko la ardhi huko Tibet
Uharibifu kutokana na tetemeko la ardhi huko TibetPicha: AP/picture alliance

Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 6.8 kwenye kipimo cha Richter lililotokea asubuhi ya leo huko Tibet, limesababisha vifo vya karibu watu 95 huku wengine 130 wakiwa wamejeruhiwa.  Shirika la utafiti wa Jiolojia la Marekani limesema tetemeko hilo lilikuwa kubwa zaidi hadi kipimo cha 7.1.

Maafisa wa eneo hilo wamesema inaaminika kuwa watu wengine wengi bado wamenaswa chini ya vifusi kutokana na mitetemeko mingine iliyofuata na kulitikisa eneo la magharibi mwa China hadi nchi jirani za Nepal, Bhutan na India ambako hakujaripotiwa maafa yoyote hadi sasa.

Soma pia: Tetemeko kubwa la ardhi laua karibu watu 100 Tibet

Takriban matetemeko 50 yalishuhudiwa ndani ya masaa matatu baada ya tetemeko hilo kubwa la ardhi, na eneo ulipo mlima mrefu zaidi duniani wa Everest upande wa China lilifungwa ili kuzuia maafa zaidi. Mamlaka zimeeleza kuwa msimu huu wa baridi kunakuwa hakuna watalii wengi hasa wale wanaopenda kupanda milima. Shirika la habari la serikali ya China CCTV limeeleza kuwa karibu nyumba 1,000 zimeharibiwa na tetemeko hilo.

Juhudi za uokoaji zinaendelea

Waokoaji wakiwatafuta manusura baada ya tetemeko la ardhi huko TibetPicha: AP/picture alliance

Waokoaji wanaendelea kuwasaka manusura kwenye vifusi vilivyofukia majumba katika moja ya kijiji kilichoharibiwa vibaya cha Tingri katika mji wa Xigaze unaopatikana takriban kilomita 380 kutoka Lhasa, ambao ndio mji mkuu wa Tibet.

Wizara ya China inayohusika na usimamizi wa majanga imesema takriban wafanyikazi 1,500 wa kikosi cha zimamoto na uokoaji pamoja na askari 200 wametumwa eneo hilo ili kusaidia zoezi la uokoaji.

Rais wa China Xi Jinping ameitoa wito wa kufanyika juhudi zote zitakazofanikisha kuokoa maisha ya watu, kupunguza idadi ya majeruhi na kuwapa makazi mapya wale wote ambao nyumba zao zimeharibiwa na janga hilo, huku akimtuma Makamu Waziri Mkuu Zhang Guoqing kuongoza shughuli hiyo huko Tibet ambako wanaishi watu wapatao 800,000.

Kiongozi wa kiroho wa Tibet Dalai Lama amesema siku ya Jumanne kuwa amehuzunishwa sana na tukio hilo na alikuwa akiwaombea waliofariki pamoja na majeruhi wa tetemeko hilo kubwa la ardhi.

(Vyanzo: DPA, AFP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW