Zaidi ya watu 90 wauawa katika shambulizi Mogadishu
28 Desemba 2019Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Ahmed Awad amesema waliouawa ni pamoja na wanafunzi wengi na raia wa wawili wa Uturuki. Ripoti ya shirika moja la kimataifa linalofanya kazi nchini humo na ambalo halikutaka kutajwa jina, imesema idadi ya vifo ni zaidi ya 90.
Mbunge mmoja wa Somalia pia amesema ameambiwa kuwa idadi ya vifo ni zaidi ya 90, wakiwemo polisi 17. Afisa polisi, Ahmed Bashane amesema kuwa takriban watu 100 wameuawa katika shambulizi hilo baya kabisa kushuhudiwa tangu miaka miwili iliyopita.
Dahir Elmi, afisa katika hospitali ya mji ya Shafi, amethibitisha kuwa watu wanane wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa. Hospitali nyingine ya Medina tayari imesharipoti vifo 73. Bashane amesema pia kuna hospitali nyingine ambazo zimepokea maiti na zaidi ya watu 100 waliojeruhiwa.
Abdikadir Abdirahman Haji Aden, mwanzilishi wa kampuni inayotoa huduma za magari ya wagonjwa ya Aamin, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba zaidi ya watu 125 wamejeruhiwa katika shambulizi hilo.
Baada ya shambulizi kutokea, Sabdow Ali, mwenye umri wa miaka 55 anayeishi kwenye eneo la karibu na lilipotokea shambulizi hilo, amesema aliondoka nyumbani kwake na alihesabu miili ya watu 13.
Akizungumza na waandishi habari katika eneo ambako shambulizi limetokea, Meya wa Mogadishu, Omar Muhamoud amesema serikali imethibitisha kwamba takriban raia 90 wameuawa na wengine wengi wamejeruhiwa.
Uturuki imekuwa mfadhili mkubwa wa Somalia tangu nchi hiyo ilipokumbwa na baa la njaa mwaka 2011 na pamoja na serikali ya Qatar zimekuwa zikifadhili miradi kadhaa ya miundombinu na afya nchini humo. Mwaka 2017, Uturuki ilifungua kambi ya jeshi mjini Mogadishu kwa ajili ya kuwapatia mafunzo wanajeshi wa Somalia.
Hakuna aliyejitokeza kudai kuhusika na shambulizi hilo baya kabisa kushudiwa Mogadishu katika kipindi cha miaka miwili. Kundi la itikadi kali la Al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda aghalabu hufanya mashambulizi ya aina hiyo, ukitaka kuiondoa madarakani serikali inayotambuliwa na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Shambulizi baya la mwisho kutokea Somalia lilikuwa la Oktoba mwaka 2017 wakati lori lililokuwa na mabomu lilipolipuka karibu na lori la mafuta mjini Mogadishu na kusababisha moto na kuwaua karibu watu 600.
Katika miezi ya hivi karibuni, serikali ya Somalia ilidai kuwa hali ya usalama imeimarika nchini humo, baada ya kuongeza wafanyakazi wa usalama pamoja na kuimarisha mfumo wa kuwafuatilia watu.
(AFP, AP, DPA, Reuters)