Zaidi ya watu milioni 800 duniani wanaugua kisukari
14 Novemba 2024Ripoti ya matokeo ya utafiti huo iliochapiswa kwenye jarida la afya la The Lancet, imebainisha kuwa mnamo mwaka 2022, kulikuwa na takriban watu milioni 828 wenye umri wa miaka 18 na zaidi waliokuwa wakiugua aina ya 1 na ya 2 ya kisukari kote duniani.
Ripoti hiyo imeendelea kusema kuwa miongoni mwa watu wazima wenye umri wa miaka 30 na zaidi, watu milioni 445 au asilimia 59 hawapokei matibabu.
Idadi ya awali ya wagonjwa wa Kisukari
Awali, WHO ilikuwa imekadiria kuwa takriban watu milioni 442 wanaugua kisukari,ugonjwasugu wa kimetaboliki unaohusisha viwango vya sukari ya damu ambao unaweza kuharibu moyo, mishipa ya damu pamoja na viungo vingine vya mwili ikiwa hautatibiwa.
Utafiti huo pia umebainisha kuwa kiwango cha kisukari duniani kimeongezeka maradufu tangu mwaka 1990 kutoka 7% hadi 14%, kutokana na ongezeko kubwa la ugonjwa huo katika nchi za kipato cha chini na kati.
Kuna pengo kubwa la matibabu kati ya mataifa mbali mbali
Lakini ingawa kuna visa zaidi vya ugonjwa huo, viwango vya matibabu katika maeneo hayo bado havijaongezeka pakubwa wakati ambapo hali imeimarika kwenye baadhi ya mataifa yenye mapato ya juu na kusababisha pengo kubwa la matibabu.
Gharama ya matibabu ya Kisukari iko juu mno
Jean Claude Mbanya, profesa katika chuo kikuu cha Yaounde nchini Cameroon, amesema katika sehemu za kusini mwa jangwa la Sahara kwa mfano, ni kati ya asilimia 5-10 ya wale wanaokadiriwa kuugua Kisukari wanaopata matibabu . Mbanya ameongeza kuwa kutibu ugonjwa wa Kisukari aidha kwa kutumia dawa ama Insulini kunaweza kuwa ghali mno.
Mbanya amesema idadi kubwa ya watu wanakabiliwa na hatari ya athari mbaya za afya.
Utafiti huo ni wa kwanza wa kimataifa wa makadirio ya matibabu
Waandishi wa ripoti hiyo wanasema utafiti huo ni uchambuzi wa kwanza wa kimataifa kujumuisha viwango na makadirio ya matibabu kwa nchi zote na kwamba umezingatia zaidi ya tafiti 1,000 zilizowahusisha zaidi ya watu milioni 140.
Ufafanuzi wa ugonjwa wa Kisukari
Ugonjwa wa kisukari ulifafanuliwa kama kuwa na viwango vya juu vya sukari katika damu baada ya kutokula au kunywa kitu chochote isipokuwa kunywa maji tu kwa saa kati ya nane hadi 12, pamoja na viwango vya juu vya chembechembe za sukariaina ya glucose iliyoganda kwenye haemoglobin katika seli nyekundu za damu zinazosafirisha hewa ya oksejeni mwilini, vyote ambayo ni vigezo vya utambuzi wa ugonjwa huo ama kwa kutumia dawa za kisukari.
WHO: Ugonjwa wa kisukari waongezeka duniani
Ripoti hiyo pia imesema vipimo vyote viwili vilitumika ili kuzuia kupuuza viwango katika sehemu za dunia, hasa Asia ya Kusini, ambapo matumizi ya kipimo cha sukari katika damu baada ya kutokula wala kunywa kitu chochote isipokuwa maji kwa saa kati ya 8 hadi 12 yanakosa kutambua wanaougua.
Ingawa utafiti huo haukuweza kutenganisha aina ya 1 na ya 2 ya ugonjwa huo wa Kisukari, ushahidi wa awali umeonesha kuwa watu wazima wanaugua zaidi kisukari aina ya 2, ambayo inahusishwa na uzito wa mwili kupita kiasi pamoja na lishe duni.