1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu robo bilioni wateswa na njaa duniani

3 Mei 2023

Ripoti ya muungano wa mashirika ya kiutu inaonesha mwaka 2022 ulishuhudia watu milioni 258 wakikabiliwa na njaa kali katika mataifa mbali mbali ya dunia.

Angola Dürre
Picha: Thomas Schulze/dpa/picture-alliance

Zaidi ya robo bilioni ya watu katika nchi 58 wamekabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula mwaka jana, kufuatia changamoto mbali mbali zilizoiandama dunia ikiwemo janga la Uviko-19 na mabadiliko ya tabia nchi. Hayo yamebainishwa kwenye ripoti iliyochapishwa  na muungano wa mashirika ya kiutu.

Ripoti kuhusu mgogoro wa chakula duniani imechapishwa na muungano wa mashirika ya kiutu ulioanzishwa na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya na inasema kwamba ukosefu wa usalama wa chakula katika kipindi cha mwaka jana ulisababishwa na migogoro,mabadiliko ya tabia nchi,athari za janga la Uviko-19 pamoja na vita nchini Ukraine.

Ripoti hiyo ikizungumzia namna hali halisi ilivyokuwa katika mataifa mbali mbali imeonesha kwamba watu walikabiliwa na njaa kali na hata kutokea vifo katika nchi saba ambazo ni Somalia, Afghanistan, Burkina Faso, Haiti, Nigeria, Sudan Kusini pamoja na Yemen.

Picha: Sam Mednick/AP Photo/picture alliance

Watu milioni 258 walihitaji msaada wa haraka wa chakula mwaka 2022 na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amebaini kwamba ripoti iliyochapishwa inaonesha idadi ya watu waliokabiliwa na njaa kali na ukosefu wa usalama wa chakula  na mahitaji ya dharura ya chakula iliongezeka kwa mwaka wa nne mfululizo hali ambayo inaonesha kushindwa kwa ubinadamu kutimiza malengo ya Umoja wa Mataifa ya kuimaliza njaa.

Ama mkurugenzi wa ofisi ya masuala ya dharura katika shirika la Umoja huo wa Mataifa la chakula na kilimo Fao- Rein Paulsen amesema.

''Takwimu za hivi sasa juu ya hali ya ukosefu mkubwa wa usalama wa chakula duniani inaonesha hali ya mashaka makubwa sana''

Paulsen amesema kuzorota kwa hali ya mambo kumechangiwa na matatizo mbali mbali  ikiwamo vita vya Ukraine ambavyo vilisababisha athari kubwa katika biashara ya ulimwengu ya mbolea, ngano,mahindi na mafuta ya kupikia ya alizeti.Na athari hizo zilikuwa mbaya zaidi katika nchi masikini ambazo zinategemea kuagiza chakula kutoka nje.

Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

''Kwetu sisi kuna msururu wa nchi zilizoorodheshwa kwenye ripoti hii ambazo zinategemea uagizaji chakula na ambazo ni nchi masikini. Na kwahivyo ni wazi wakati bei zimebadilika,na kuwa za juu nchi hizo zimekuwa zikiathirika kwa kiwango kikubwa sana''

Ametowa mwito wa kufanyika mageuzi ya msingi ili fedha zaidi zitumike katika kuwekeza kwenye kusaidia kuimarisha kilimo kubabiliana na migogoro ya chakula yakiweko malengo ya kuzuia migogoro hiyo kutokea.

Mwandishi Saumu Mwasimba
Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW