1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zambia yatangaza siku 21 kuomboleza kifo cha Kaunda

Josephat Charo
18 Juni 2021

Serikali ya Zambia imetangaza siku 21 za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha muasisi wa taifa hilo Kenneth Kaunda hapo jana. Kaunda anakumbukwa kama baba wa taifa na mkombozi wa Zambia.

Kenneth Kaunda | ehemaliger Präsident Sambias
Picha: Xinhua/imago images

Serikali ya Zambia iliamuru bendera zipeperushwe nusu mlingoti na imepiga marufuku matukio yote ya burudani kwa heshima ya kiongozi huyo wa zamani aliyekuwa na haiba kubwa. Rais wa sasa wa Zambia Edgar Lungu alisema Kaunda amefariki wakati ambao hawakutarajia, huku akimueleza kuwa kiongozi halisi wa Afrika.

Katibu wa baraza la waziri Simon Miti alisema katika hotuba kwa umma wa Zambia kupitia runinga kwamba Kaunda alikufa kwa amani mida ya nane unusu jana katika hospitali hiyo ya jeshi ambako alikuwa akitibiwa tangia Jumatatu.

Akifahamika sana kama KK, Keneth Kaunda alikuwa kiongozi wa chama kilichoiongoza Zambia baada ya uhuru kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Uingereza. Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, aliandika katika ukurasa wake wa twita akisema amehuzunishwa na taarifa za kifo cha Kaunda na kutuma risala za rambirambi kwa watu wa Zambia.

Makamu wa rais wa zamani wa Zambia kati ya mwaka 2001 na 2003, Enoch Kavinde, amezungumzia hivi kifo cha Kaunda.

"KK atakumbukwa na kila mtu, ndiyo, kila mtu nchini humu, marafiki na maduni, watu katika chama chake na vyama vingine, tutamkosa sana kwa kuwa alikuwa nyota iliyong'aa"

 Risala za rambirambi zamiminika

Raia wa Zambia wametoa hisia zao pia kuhusu kuondokewa na mausisi wa taifa lao. Mukela Mubiana mkazi wa mjini Lusaka alisema Kaunda alikuwa muanzilishi wa ukombozi wa Zambia na wao kama vijana watalikumbuka hilo.

Naye Manfred Mubita alisema Mungu alimtumia Kaunda kwa kiwango kikubwa sana, kiasi cha kuikomboa Zambia na kuileta nchi hiyo mahala ilipo sasa. Hakutaka kumwaga damu, hakutaka kufanya kitu chochote kwa manufaa yake binafsi. Hakuwa mtu mwenye ubinafsi," aliongeza kusema.

Yoram Siamvwa alisema Kenneth Kaunda kwake yeye hakuwa raia wa kawaida wa Zambia bali alikuwa baba wa taifa na alifanya mengi akisisitiza wapo walipo sasa kwa sababu yake yeye.

Naye Sara Mafuta alisema, "Nina huzuni sana, lakini naamani ameikamilisha safari yake ya maisha. Tunatakiwa kusherehekea uhuru aliotuletea."

Rais Cyril Ramaphosa, rais wa Afrika KusiniPicha: AFP/WHO

Afrika Kusini imetangaza siku kumi za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha Kaunda. Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alisema, "Kufariki kwa rais Kenneth Kaunda kumetusikitisha sisi kama waafrika kusini. Tunainamisha vichwa vyetu kwa huzuni na simanzi kwa kuondokewa na kipenzi chetu baba wa uhuru na umoja wa Waafrika. Tumeungana katika majonzi na familia ya Kaunda, serikali na watu wa Jamhuri ya Zambia."

Chama cha African National Congeress, ANC, cha Afrika Kusini kilimueleza Kaunda kama kiongozi jabali wa vita vya ukombozi barani Afrika. Naye rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki alimueleza Kaunda kama mtu wa watu.

Moussa Faki, rais wa kamisheni ya Umoja wa Afrika alisema Kaunda alikumbatia sana umoja wa waafrika wote, akiiweka nchi yake katika hatari kubwa kwa kutoa maficho kwa mavuguvugu ya kupigania uhuru.

Kaunda alizaliwa kama mtoto wa mwisho katika familia ya watoto wanane ya mchungaji wa kanisa la Presbyterian mnamo Aprili 28, 1924 katika misheni ya Lubwa kaskazini mwa Zambia, wakati huo ikijulikana kama Rhodesia Kaskazini.

(afp, reuters)