Zanzibar. CCM yaibuka na ushindi Zanzibar.
2 Novemba 2005Rais wa Zanzibar ameshinda uchaguzi mkuu wa nchi hiyo siku ya Jumanne baada ya uchaguzi ambao umegubikwa na ghasia , lakini upande wa upinzani umedai kuwa kulikuwa na udanganyifu mkubwa na kuahidi kuwa watafanya maandamano ikiwa ni ishara ya kuongezeka kwa mzozo wa kisiasa katika eneo hilo tete la Tanzania.
Majeshi ya usalama yalipambana na waungaji mkono wa upinzani siku nzima jana na wafanyakazi wa kutoa mashirika ya kutoa misaada wamesema kuwa mtu mmoja alipigwa risasi na kufa wakati wa ghasia hizo katika kisiwa cha Pemba.
Polisi na waandishi wa habari hawakuweza kuthibitisha ripoti iliyotolewa na chama cha upinzani cha Civic United Front, CUF kuwa watu wapatao watano wakiwa wanachama wao wameuwawa katika kisiwa cha Pemba.
Baada ya kutangazwa matokeo ya ushindi kwa chama tawala cha CCM, maelfu ya waungaji mkono chama hicho waliingia mitaani wakiwa wamevalia rangi za kijani na njano wakipiga honi , kupepea bendera za chama chao na kucheza. Hata hivyo polisi hawakuingilia kati.
Wakati huo huo Marekani jana imeutaka uongozi wa serikali ya Zanzibar kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya madai ya udanganyifu katika kura iliyofanyika katika kisiwa hicho hapo Jumapili.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Sean McComarck amesema kuwa serikali hiyo itahimizwa kufanya uchunguzi kuhusu madai yoyote ya udanganyifu kwa kina na uwazi.