Zanzibar kuanzisha mkakati wa "Halal Tourism” kukuza utalii
23 Machi 2026
Utalii Halali ambao wanasema unafuata misingi ya haki na kutokuwa na mizengwe yoyote, unalenga kuwavutia watalii kutembelea visiwa hivyo na kuona maeneo ambayo historia yake ina uhusiano mkubwa na masuala ya kidini. Utalii kama huu umekuwa ukishuhudiwa katika maeneo mbalimbali duniani ikiwamo huko Jerusalem, Vatican, Morocco na hata Uturuki ambako watalii hutembelea na kujionea masuala yenye kukumbusha matukio na historia za kidini.
Utalii ni moja ya nguzo muhimu katika uchumi wa Zanzibar na sehemu kubwa ya mapato yake yanatokana na sekta hii yenye historia kubwa. Kwa mujibu wa takwimu kutoka kwa mamlaka zinazohusika na sekta hiyo, mnamo mwaka 2025 pekee, visiwa hivi vilipokea zaidi ya watalii laki 9. Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka katika miaka ijayo kutokana na mipango inayolenga kuboresha na kutanua miundombinu ya usafiri.
Wakazi wengi visiwani humo wanaona kwamba kuwepo kwa mazingira rafiki pamoja na utulivu wa kimazingira ni moja ya sababu inayoendelea kuwavutia wageni wengi kutembelea visiwa vya Zanzibar.
"Kuhamasisha kwamba Wazanzibar wamejawa na upendo kila watalii wanavyoona upendo ambao Zanzibar tunao, namna ya kujumuika kwa pamoja wa hali ya nchini hali ya juu maana kila mtalii anahamasika kuja kuona upendo ambao tunao katika kisiwa chetu cha Zanzibar kwa hiyo Zanzibra ni nche yenye amani kwa hiyo watalii wanavutika kulingana na tunavyoishi."
Juhudi za serikali katika kukuza aina hii ya utalii
Katika juhudi za kuimarisha sekta ya utalii, hivi sasa mamlaka imeanzisha mpango mpya wa kusukuma mbele ajenda ya utalii mpya unaojulikana kama utalii halali, neno ambalo huenda ni geni masikioni mwa wengi, lakini ukweli wa mambo ni kwamba aina hii ya utalii imekuwa mtaji mkubwa katika maeneo mengi duniani.
Baadhi ya maeneo ulimwenguni yanaona utalii wa aina hii kama kielelezo cha kuikumbusha jamii kuhusu kule ilikotoka na hatma yake katika siku zijazo. Zanzibar inasema kupitia utalii Halali inakusudia kufika mbali, hasa ikitambua kuwa mambo yanayofungamana na historia pamoja na ustarabu wa kidini bado yapo visiwani humo.
Kulingana na Katibu Mtendaji wa kamisheni ya utalii visiwani Zanzibar , Arif Abba, mamlaka visiwani humo inakusudia kuufikisha mbali zaidi utalii huu ingawa safari yake ya kufikia kilele cha mafanikio bado ni ndefu. Anasema anaunga mkono wazo hilo na sasa hivi angependa tu kuishukuru serikali kwa kuwa imeweza kuona fursa kwenye suala hili la halal tourism.
" Kwa vile tunaona watu wengi sana wanaenda miji kama ya Vatican, Jerusale, lakini pia hapa Zanzibar tunavivutio vingi sana ambavyo vinamichepuko kutokana na dini, kutokana na watu walikuja hapa kueneza dini, kwa hiyo sasa hivi tumeanza kutangaza suala nzima la halal tourism," alisema bwana Abba.
Vivutio vya Zanzibar kuwavuta watalii zaidi
Kwa kawaida, Zanzibar ni kisiwa kinachotajwa kuwa na vivutio vya aina nyingi ambavyo hupelekea wageni kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni kuja visiwani humo kwa ajili ya kushuhudia kwa macho yao. Ukiweka kando utalii huu halali, kisiwa hiki pia ni maskani ya aina nyingine za utalii ikiwamo ule unahusisha magofu ya kale na utamaduni wa wakazi wake. Mkazi huyo aliyefunga safari kutoka bara na kwenda Zanzibar kwa ajili ya kujionea hali ya mambo anasema kuna vitu vikumbwa na vizuri hapa Zanzibar, hususani hapa Unguja na hata sisi watu wa ndani hatuvijui.
"Mimi binafsi napanga baada ya safari hii itabidi nirudi na familia yangu kwa ajili ya kushuhudia mambo makubwa haya, kwanza soko la utumwa na mengineyo. Nawaomba watu waje Zanzibar kuna maaneo mengi mazuri ya kihistoria, " alisema raia huyo.
Utalii unaoheshimu mazingira
Utalii unaoharibu mazingira umekuwa ukipigwa vita karibu kote duniani na mamlaka zinazohusika na eneo la ukuzaji utalii zinasema jambo hilo linatiliwa mkazo. Wengi wanasema mazingira ndiyo nguzo muhimu ya kuweza kuendeleza utalii halal na kwamba mazingira ya asili na utamadani wake ndiyo mwelekeo unawasukuma watalii wengi kufunga safari kuja kujionea.
Mkazi mmoja ambaye ni muumini wa utalii wa kutunza mazingira anaamini kwamba bila kutilia mkazo eneo la uhifadhi wa mazingira, itakuwa vigumu kusukuma mbele ajenda hii ya utalii halali .
" Tunaweza tukatunza mazingira, tukatunza mazingira, tukatunza vifaa vyetu vyote kwa ujumla ili tuweze kutengeneza miundombinu mizuri katika maeneo yetu. Mazingira haya yasiharibiwe yaani waendelee kuweka mfumo huu huu wa kukarabati, huwezi kutoa milango iliyokuwepo uweke milango mipya ya kisasa tunakuwa tunaharibu madirisha," alisisitiza mkazi huyo.
Kama sehemu ya kudumisha utamaduni na historia yake, utalii halali ni sehemu inayowezesha familia kukusanyika pamoja ili kutafakari na fursa ya kusambaza upendo na udugu. Mambo kama hayo yanadhihirika zaidi wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ambapo waumini hukusanyika pamoja kwa ajili ya kupata futari na nasaha kutoka kwa viongozi wa dini.
Katika kipindi cha mwezi wa ramadhani mwaka huu, zaidi wa waumini 15,000 walikusanyika katika uwanja wa amani Zanzibar wakifuturu pamoja. Tukio hilo linatajwa kuvunja rekodi iliyowekwa awali nchini Ethiopia ambako watu 7,000 walikusanyika pamoja.
Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi aliliita tukio hilo kuwa la aina yake akisema ni kichocheo kinachosukuma mbele ajenda ya uimarishaji amani ambayo ndani yake hukuza utalii ikiwamo utalii halali.
Kwa hivi sasa Zanzibar imeanza safari ya kuutangaza zaidi utalii halali ikitarajia kwamba katika siku za usoni itakuwa kinara katika sekta hii. Arif Abba ambaye ni katibu mtendaji wa kamisheni ya utalii anasema licha ya aina hii ya utalii kuwa mpya visiwani humo, hiyo haimanishi safari ya kuelekea kilele cha mafanikio itaishia njiani.