1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya CAG Zanzibar yabaini madudu makubwa sekta ya umma

24 Mei 2021

Kwa mara ya kwanza katika miaka ya karibuni, mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hisabu za serikali visiwani Zanzibar amekabidhi ripoti yake hadharani kwa rais wa visiwa hivyo, huku akibainisha upotevu mkubwa wa fedha za umma.

Tansania | Zanzibar Revolution Day
Picha: Salma Said/DW

Kwa mujibu wa mkaguzi mkuu wa hisabu za serikali Othman Abbas Ali, taasisi, wizara na mashirika mengi ya serikali yameshindwa kuthibitisha matumizi ya mabilioni ya fedha za walipa kodi, jambo linaloashiria kiwango kikubwa cha ufisadi.

"Tukiendelea na utaratibu huu, hatuwezi kuijenga nchi. Tuna miradi mingi ya maendeleo, tuna huduma za jamii nyingi: maji, elimu, afya. Tukiruhusu fedha hizi zote zipotee, hatutofika," alisema rais Hussein Ali Mwinyi baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo ya ukaguzi.

Soma pia: Wazanzibari wahimizwa kudumisha amani

Miongoni mwa taasisi hizo ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, ZSSF, ambao mkurugenzi na bodi yake walifutwa kazi na Rais Mwinyi hata kabla ya ripoti hii kuwasilishwa.

Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwa na makamu wake wa kwanza, Othman MAsoud Othman.Picha: Glenn Carnell/State House Zanzibar

"Ukaguzi wangu pia umeshindwa kupata uthibitisho wa shilingi bilioni 1.190 ikiwa ni gharama za awali za utekelezaji wa  Mji Mpya wa Kwahani. Tumedai, tumekaa nao ZSSF, lakini taratibu zao bado wapo kwenye michakato. Na mimi naliripoti kama nilivyolibaini," alisema CAG Othman.

Ukaguzi huo pia umegunduwa upotevu mkubwa wa fedha za umma kupitia mfumo wa ukusanyaji kodi, kwa sababu ya kutokurikodiwa vyema, licha ya taratibu na kanuni za fedha serikalini kulazimisha kuwekwa rikodi hizo.

Watendaji wajaribu kuzuwia shughuli za ukaguzi

CAG Othman alisema kwamba licha ya kuwasiliana na wizara ya fedha kuhusiana na mianya hiyo ya upotevu wa fedha, hakuwa amejibiwa hadi anawasilisha ripoti yake siku ya Jumapili.

Miongoni mwa mengi aliyobanisha mkaguzi huyo, ni hatua ya wizara inayohusika na vikosi vya usalama kununuwa magari matatu kwa dola laki tano za Kimarekani, shilingi bilioni 1.3 zilipotea kwenye wizara ya kilimo, shilingi bilioni 2.59 zilizolipwa na wizara ya uvuvi kwa ajili ya boti ambazo hazijapatikana tangu Julai 2020, mbali ya tuhuma za kuzuiwa na wahusika wa baadhi ya wizara serikalini kutofanya ukaguzi wake.

Ripoti ya CAG yazua gumzo Tanzania

03:12

This browser does not support the video element.

Soma pia: Mwinyi: Tubadilishe mfumo wa uendeshaji wa mashirika

Kuhusu hilo, Rais Mwinyi aliamuru mara moja mkaguzi huyo kurejea kwenye maeneo hayo kuendelea na ukaguzi, huku akiahidi kuchukuwa hatua kali:

"Mkaguzi mkuu akaendelee pale aliposimamishwa kuanzia kesho (Mei 24). Wahusika wote watowe ushirikiano wa mia kwa mia. Nisisikie tena kama fulani kazuwia ukaguzi," aliamuru rais Mwinyi, huku akiahidi kuchukuwa hatua kali.

Ama endapo ahadi hii ya Rais Mwinyi kurejesha nidhamu ya matumizi za umma serikali itafanikiwa ama la, ni jambo la kusubiri na kuona.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW