Zarif na mawaziri wa Ulaya kuokoa makubaliano ya kinyuklia
15 Mei 2018Zarif alikutana na mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini kabla ya mazungumzo jioni ya leo na mawaziri wenzake kutoka Uingereza , Ufaransa na Ujerumani, nchi tatu zilizotia saini makubaliano ya kihistoria mwaka 2015 ambayo wanajaribu kuyaendeleza.
Iran imeonya kwamba inajirayarisha kuanza tena urutubishaji wa kiwango cha viwanda kwa madini ya urani , bila vizuwizi , hadi pale mataifa ya Ulaya yatakapoweza kutoa uhakikisho kamili kwamba wanaweza kuendeleza maslahi ya kiuchumi yaliyopatikana kutoka katika makubaliano hayo ya kinyuklia licha ya Marekani kurejesha vikwazo.
Zarif ametoa tathmini ya matumaini baada ya mkutano ambao ulikuwa mzuri na wenye mwelekeo pamoja na Mogherini.
"Naamini tuko katika njia sahihi kusonga mbele ili tuweze kuhakikisha kwamba maslahi ya washiriki wote waliobaki katika mpango wa pamoja wa kuchukua hatua JCPA , hususan Iran , yatalindwa na kuhakikishwa," aliwaambia waandishi habari.
Lakini wanadiplomasia wa Ulaya hawakutaka kuonesha matarajio makubwa kutoka katika mkutano huo wa leo, wakisisitiza tu kuhusu changamoto kubwa ya kutafuta njia kukwepa vikwazo vya Marekani vya biashara ya nje na Iran, ambayo inafika kila mahali duniani.
Bado kutakuwa na utata
"Hakuna suluhisho moja la miujiza, kutakuwa na matukio yenye utata, na magumu katika ngazi ya Umoja wa Ulaya na kitaifa, kwa hiyo itachukua muda," afisa mwandamizi wa Umoja wa ulaya alisema.
Umoja wa Ulaya unasisitiza kwamba makubaliano hayo yanafanyakazi, wakielekeza katika uchunguzi wa mara kwa mara wa Umoja wa Mataifa unaofanya tathmini ya utekelezaji wa taifa hilo la Kiislamu kwa upande wake wa makubaliano, na msemaji wa Mogherini Maja Kacijancic akiliambia shirika la habari la AFP kabla ya kuwasili kwa Zarif kwamba " tunapawa kufanya kila linalowezekana kuulinda mkataba huo".
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaonesha msimamo wa pamoja katika kulinda makubaliano hayo na Iran wakati walipokutana kwa chakula cha usiku kabla ya mkutano mjini Sofia siku ya Jumatano, afisa huyo alisema.
Mogherini na mkuu wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker wanaainisha kwa viongozi hatua gani kundi hilo la mataifa linaweza kuchukua kukinga maslahi yake ya kiuchumi nchini Iran.
Makampuni ya Ulaya , hususan yale ya Ufaransa na Ujerumani, yalikimbilia kuwekeza nchini Iran kufuatia makubaliano hayo ya mwaka 2015 , ambayo Tehran ilikubali kusitisha mpango wake ili kuondoa vikwazo vikali vya kiuchumi vya kimataifa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman