1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ZEC yatangaza kukamilika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu

Salma Said 27 Oktoba 2025

Tume ya uchaguzi Zanzibar ZEC imetangaza kukamilika kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu ambapo kura ya mapema itafanyika kesho Jumanne kote visiwani Zanzibar na siku ya pili ya uchaguzi itakuwa Jumatano ya wiki hii.

Tansania Sansibar | Vorsitzender der Wahlkommission George Joseph Kazi
Picha: Salma Said/DW

Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji George Joseph Kazi amesema kura ya mapema ambayo inapingwa na chama cha ACT-Wazalendo itafanyika mapema kama ilivyopangwa na itafuatiwa na upigaji kura wa jumla hapo Oktoba 29 ambapo matayarisho yote yameshakamilika.

Jaji kazi amewataka waangalizi wa uchaguzi kufuata sheria ya muongozo ikiwemo kutoingilia kazi za ZEC na kuwaeleza miongozo iliyopo kisheria.

Mwenyekiti huyo amaesema kifungu cha 100 (1) cha Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018 kimeipa uwezo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kualika taasisi za ndani zilizosajiliwa na Waangalizi wa kimataifa kwa madhumuni ya kufanya uangalizi wa uchaguzi.

"Tume imeshatoa vibali vya uangalizi kwa taasisi 61 (51 taasisi za ndani na 10 taasisi kutoka nje ya nchi) ambazo zimekidhi vigezo. Kupata kibali hiki kwa taasisi hizo ni ishara ya imani kubwa ambayo Tume na Taifa kwa ujumla imeweka kwenu katika kulinda misingi ya uwazi na demokrasia” amesema Jaji Kazi. Amewambia waangalizi wa uchaguzi kuwa wana jukumu muhimu la kufuatilia mwenendo wa shughuli za uchaguzi na kutoa taarifa huru kuhusu namna uchaguzi unavyotekelezwa.

Wananchi wa Jimbo la Kikwajuni wakitizama majina yao yalioorodheshwa katika vituo cha vya kupigia kura katika shule ya Haile Sellasie Mkoa wa Mjini wa Magharibi Zanzibar.Picha: Glenn Carnell/State House Zanzibar

"Hata hivyo, mamlaka hayo yana mipaka ambayo inalenga kuhakikisha hamuingilii kazi za wasimamizi wa uchaguzi, wagombea au wapiga kura.

Jaji Kazi ametoa wito kwa waangalizi kuwakumbusha kutekeleza wajibu wao kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 105 (1) cha Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018, ambacho kinabainisha wajibu ufuatao kwa Waangalizi wa Uchaguzi huu wa 2025.

Akiyataja mambo ambayo yameainishwa kisheria ni Kuendesha majukumu yao kwa uangalifu, uhuru na malengo, kuheshimu Sheria za Zanzibar na za Jamhuri wa Muungano wa Tanzania; Kutoingilia au kuzuia shughuli za utendaji wa Uchaguzi, na Kulinda siri za upigaji kura.

Majukumu mengine aliyowaambia waangalizi hao ni Kuipatia Tume nakala ya maandishi na taarifa mtakazoziandika na maelezo mtakayoyatoa. Vituo vya kura ya mapema vitafunguliwa saa moja asubuhi na kufungwa saa 10 jioni na matokeo ya urais yatatangazwa ndani ya saa 72.

Makundi ambayo yamepangwa kupiga kura ya kesho ni askari polisi na vikosi vya SMZ pamoja na watendaji wa tume ya uchaguzi ambao watasimamia uchaguzi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW