ZEC yatangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio Z'bar
22 Januari 2016Katika taarifa aliyoisoma mchana wa leo kupitia Shirika la Habari la Serikali (ZBC) Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jecha Salum Jecha, alisema uchaguzi huo utawahusisha nafasi za urais, uwakilishi na udiwani na kwamba hakutakuwa na uteuzi mpya wa wagombea wala mikutano ya kampeni.
"Nachukua fursa hii kuwatangazia rasmi wananchi kwamba Tume ya Uchaguzi katika kikao chake kilichofanyika tarehe 21 Januari 2016 imeamua kwamba uchaguzi wa marudio utafanyika siku ya Jumapili ya tarehe 20 Machi 2016," alisema Jecha katika taarifa yake hiyo fupi.
Taarifa za kutangazwa kwa tarehe hiyo zilishasambaa tangu asubuhi kwenye mitandao ya kijamii, baada ya watu kuripoti idadi kubwa ya vikosi vya ulinzi na usalama kwenye mitaa mbalimbali mjini Zanzibar.
Chama cha Wananchi (CUF) kupitia kwa kaimu wake wa habari, Ismail Jussa, kimeiambia Deutsche Welle kwa njia ya simu kwamba kilichofanywa na Jecha ni muendelezo wa kuvunja sheria za nchi.
"Hakuna mahala popote ndani ya Katiba na sheria za nchi yetu, ambapo panatolewa mamlaka kwa tume ya uchaguzi kufuta uchaguzi. Kwa hivyo, kinachoendelea ni kuendeleza haramu tu kwa sababu ni kawaida unapofanya haramu moja inabidi ufanye haramu nyengine nyingi sana kuhalalisha haramu yako uliyoanzia," alisema Jussa kwa njia ya simu.
Pamoja na hayo, CUF ilitoa wito kwa watu kutulia na kungojea msimamo rasmi wa chama hicho kinachodai kuwa mgombea wake wa urais kwenye uchaguzi uliofutwa, Maalim Seif Sharif Hamad, alishinda uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba.
Mzozo wa kisiasa na kisheria uliotokana na kufutwa kwa uchaguzi huo ulipelekea mazungumzo ya miezi miwili kati ya mgombea wa urais wa CUF, Maalim Seif, na mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohammed Shein, sambamba na marais wastaafu wa Zanzibar, lakini yalivunjika wiki iliyopita, huku Maalim Seif akisema wenzake hawakuwa na azma ya kuukwamua mkwamo uliopo na akimtolea wito Rais John Magufuli wa Jamhuri ya Muungano kuingilia kati.
Kufutwa kwa uchaguzi
Katika taarifa aliyoisoma leo, Jecha amerejea msimamo wake wa awali kwamba kufutwa kwa uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba kulitokana na kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi huo, ingawa kwa mara nyengine tena - kama ilivyokuwa kwa tangazo lake la tarehe 28 Oktoba kufuta uchaguzi - mwenyekiti huyo wa ZEC hakueleza kurejewa kwa uchaguzi huo ni chini ya kifungu kipi cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, wala masuala mengine yanayobishaniwa kama vile uhalali wa bajeti ya uchaguzi huo mpya na kutokuaminika kwa tume yake na wadau wa uchaguzi wenyewe.
Badala yake, Jecha alisema tokea kufutwa kwa uchaguzi huo, tume yake imekuwa ikiendelea na hatua mbalimbali za maandalizi ya uchaguzi wa marudio ikiwemo kufanya vikao ili kuwezesha kufanikisha uchaguzi huo, na alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananch, viongozi na wanachama wa vyama vya siasa kwa ustahamilivu na utulivu mkubwa waliouonesha katika kipindi chote cha kusubiri tume kukamilisha kazi yake.
"Ni dhahiri kuwa ustahamilivu huo umeendelea kuiweka nchi yetu katika hali ya amani na utulivu," alisema Jecha.
Wazanzibari walipiga kura siku moja na Watanzania wote kuwachagua viongozi wa mbali mbali ikiwemo nafasi ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, rais wa Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani, lakini uchaguzi uliofutwa ni ule uliohusu Zanzibar pekee.
Kauli ya Jecha ilipigwa vikali na wanasiasa, wanaharakati na wanasheria kutoka Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) kwa madai kuvunja Katiba na Sheria za Uchaguzi za Zanzibar.
Mwandishi: Salma Said/DW Zanzibar
Mhariri: Mohammed Khelef