1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ZEC yatupa pingamizi dhidi ya Mansoor

Salma Said10 Septemba 2015

Muda mchache kabla ya Chama cha Wananchi (CUF) kuzindua rasmi kampeni za uchaguzi mkuu visiwani Zanzibar, Tume ya Uchaguzi ya huko (ZEC) ilitupilia mbali kesi za kupinga uteuzi wa baadhi ya wagombea.

Mansoor Yussuf Himid
Mansoor Yussuf HimidPicha: DW/M.Khelef

Katika maamuzi yake, ZEC ilisema kuwa mashitaka dhidi ya mmoja wa wagombea wa CUF waliowekewa pingamizi, Mansoor Yusuf Himid, kwa madai ya kufanya udanganyifu katika hati yake ya kiapo, hayana msingi na Tume ikamruhusu kugombea uwakilishi katika jimbo jipya la Chukwani, magharibi ya kisiwa cha Unguja.

Hata hivyo, wakili wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichoweka pingamizi hiyo, Rashid Msaraka, alisema hakubaliani na uamuzi huo na kwamba angelikata rufaa.

ZEC ilisema kabla ya kufikia maamuzi ya kutupa pingamizi dhidi ya Mansoor, wanasheria wake waliangalia kumbukumbu ya kesi ya aina hiyo iliyotokea mwaka 2010. Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo la Chukwani, Iddi Hussein Iddi, aliiambia Dw kwamba alizingatia yafuatayo katika kutoa uamuzi wake:

  • Je, mgombea amefanya udanganyifu katika hati zake?
  • Je, maneno marisau na risasi yana maana moja?

Kwa uamuzi wa ZEC, tuhuma zote hizo hazimuondolei uhalali Mansoor kugombea kwa sababu kimsingi hati mgombea huyo alijaza fomu zote kwa mujibu wa sheria na taratibu za uchaguzi na pia hakuidanganya mahakama na vile vile risasi na marisau ni vitu viwili hivyo vina maana moja kwa mujibu wa sheria.

Wakili Msaraka alisema hoja yao dhidi ya Mansour bado ni za msingi na kwamba mgombea huyo ambaye ni mshauri maalum wa mgombea wa urais kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alifanya makosa katika kujaza hati ya kiapo.

Wakili huyo pia aliikosoa ZEC kumpa fomu Mansoor za kuendelea na shughuli za kampeni wakati wakijua hilo ni kosa, hatua ambayo ilijibiwa haraka kwa ZEC kumtaka Mansoor kurejesha fomu hiyo, naye akaahidi kufanya hivyo.

Mwandishi: Salma Said/DW Zanzibar
Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW