Zelenskiy ataka kumaliza vita mwaka ujao
16 Novemba 2024Rais Volodymyr Zelenskiy amesema Ukraine lazima ifanye kila iwezalo kuhakikisha vita na Urusi vinamalizika mwaka ujao kupitia diplomasia, akitoa maoni yake katika wakati muhimu baada ya ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa urais wa Marekani na mafanikio ya kivita ya Urusi.
Hata hivyo, Zelenskiy alisema Rais wa Urusi, Vladimir Putin, hana nia ya kufikia makubaliano ya amani, na alieleza kuwa siyo rahisi kwa Moscow kukaa mezani kwa mazungumzo huku ikiendelea kupigana.
"Kutoka upande wetu, lazima tufanye kila kitu ili vita hivi vimazike mwaka ujao, vimazike kwa njia za kidiplomasia," Zelenskiy alisema katika mahojiano na redio ya Ukraine yaliyotangazwa Jumamosi.
Balozi wa Moscow katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva alisema Alhamisi kuwa Urusi itakuwa tayari kwa mazungumzo ya kumaliza vita ikiwa yataanzishwa na Trump, ingawa aliongeza kuwa mazungumzo hayo yanapaswa kutambua "hali halisi katika uwanja wa vita".
Soma pia: Zelensky aelezea kusikitishwa na mazungumzo ya Scholz, Putin
Moscow hutumia neno hilo kumaanisha kwamba Ukraine italazimika kukabidhi maeneo manne ambayo vikosi vya Russia vimeyakamata kwa sehemu na ambayo Urusi imeyadai kwa ukamilifu wake.
Zelenskiy amesisitiza mara kadhaa tangu uvamizi kamili wa Urusi Februari 2022 kwamba amani haiwezi kupatikana hadi vikosi vyote vya Urusi vitimuliwe na maeneo yote yaliyotekwa na Moscow, ikiwemo Crimea, yarudishwe.
Hata hivyo, kurejesha mipaka ya Ukraine inayotambuliwa kimataifa ya mwaka 1991 hakukutajwa katika "mpango wa ushindi" wa rais huyo ambao aliwekwa wazi mwezi uliopita.
Zelenskiy alisema vita vinaweza kumalizika haraka chini ya Trump, ambaye mara nyingi wakati wa kampeni yake alisema angehitimisha haraka mzozo huo, bila kutoa maelezo maalum.
Zelenskiy alisema sheria za Marekani zinamzuia kukutana na Trump kabla ya kuapishwa kwake tarehe 20 Januari.
"Tutafanya kila kitu kinachotegemea sisi (ili kuhakikisha mkutano unafanyika). Tulikuwa na mkutano mzuri sana mwezi Septemba," Zelenskiy alisema, akiongeza kuwa atazungumza tu na Trump mwenyewe badala ya mwakilishi au mshauri yeyote.
Hali katika eneo la mashariki mwa Ukraine
Zelenskiy alikubali kwamba hali katika mashariki mwa Ukraine ilikuwa ngumu na Urusi ilikuwa ikipata mafanikio kwenye uwanja wa vita.
Soma pia: US kuiongezea Ukraine misaada kabla ya Trump kuingia madarakani
Vikosi vya Moscow kwa sasa vinaelekea Kurakhove, ambapo kuna kituo cha umeme wa joto kilichopo umbali wa kilomita 7 tu kutoka Pokrovsk, mji mkubwa ambao kwa sehemu kubwa ya vita umekuwa moja ya vituo muhimu vya usafirishaji na ugavi wa vifaa kwa wanajeshi wa Ukraine.
Katika medani za vita za mashariki mwa Ukraine, Urusi sasa inasonga mbele kwa kasi zaidi tangu siku za mwanzo za vita mwaka 2022.
Zelenskiy alisema hali ilikuwa ngumu kwa sababu kadhaa, mojawapo ikiwa ni kucheleweshwa upatikanaji wa msaada uliotokana na kuchelewa kwa bunge la Marekani kuidhinisha msaada huo.
Hata hivyo, alisema baadhi ya vikosi hivi sasa vitaingia kwenye mapambano.
"Ili kuizuia jeshi la Urusi, wanajeshi wapya wa akiba waliyotayarishwa na vifaa ambavyo tumekuwa tukisubiri kwa muda mrefu, sasa vitawasili," alisema.
Soma pia: Trump, Biden wazungumzia mizozo ya Ukraine na Mashariki ya Kati
Ukraine inapambana kuongeza uzalishaji wake wa silaha ili kupunguza utegemezi kwa washirika. Zelenskiy alisema Ukraine kwa sasa inatengeneza makombora manne tofauti, ambayo alisema yapo katika hatua za majaribio.