1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelenskiy kulihutubia bunge la Marekani

16 Machi 2022

Urusi imezidisha mashambulizi yake nchini Ukraine huku maroketi kadhaa yakiripotiwa katika eneo moja la makazi la Mji Mkuu Kyiev usiku wa kuamkia Jumatano.

Ukraine | Ansprache Präsident Wolodymyr Selenskyj 07.03.2022
Picha: UKRAINIAN PRESIDENT OFFICE via REUTERS

Haya yanafanyika wakati ambapo Urusi yenyewe inaendelea kukanusha kwamba inawalenga raia huku Rais wa Ukraine Volodomyr Zelenskiy akiwa anajiandaa kulihutubia bunge la Marekani, Congress Jumatano ili kuomba msaada zaidi.

Mkuu wa eneo la Kyiev Oleksiy Kuleba amesema mashambulizi yameongezeka katika mji wa Bucha ulioko kaskazini magharibi mwa mji huo mkuu, huku akidai wanajeshi wa Urusi wanajaribu kukata njia za usafiri za kutoka na kuingia Kyiev wakati wanapojiandaa kufanya mashambulizi makubwa na kuuteka mji huo. Kuleba anasema miji 12 inayoizunguka Kyiev haina huduma za maji na sita kati ya hiyo haina nguvu za umeme.

Wakati huo huo mshauri wa wizara ya usalama wa ndani ya Ukraine Anton Gerashchenko amesema kamanda wa nne wa Urusi ameuwawa katika vita hivyo vinavyoendelea. Gerashchenko ambaye alichapisha picha ya afisa huyo katika mtandao wa Telegram amesema meja jenerali Oleg Mityaev aliuwawa Jumanne wakati wa uvamizi wa mji wa Mariupol.

Kuna matumaini katika mazungumzo ya Urusi na Ukraine

Lakini licha ya mwendelezo wa uvamizi wa mji wa Mariupol, Ukraine kupitia Rais Volodomy Zelenskiy  inasema kuna fursa ya mwafaka kupatikana katika mazungumzo na Urusi.

Picha ya setlaiti inavyoonesha uharibifu katika mji wa MariupolPicha: via REUTERS

"Mikutano inaendelea na naarifiwa majadiliano yanatia moyo ila muda bado unahitajika ili maamuzi yatakayotolewa yawe kwa ajili ya nia nzuri ya Ukraine," alisema Zelenskiy.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov naye amedai mazungumzo hayo si rahisi ila kuna matumaini ya maelewano kupatikana.

Mazungumzo hayo yanaendelea wakati ambapo Rais wa Ukraine, Zelenskiy, anatarajiwa kulihutubia bunge la Marekani, Congress Jumatano kupitia njia ya video, hiyo ikiwa ni hotuba ya pili ya aina hiyo kutolewa na rais huyo katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita. Baada ya hotuba hiyo, Rais Joe Biden anatarajiwa kutangaza msaada wa ziada wa usalama kwa Ukraine wa dola milioni 800.

Hapo Jumanne, Zelenskiy, aliwahutubia viongozi wa Ulaya waliokuwa wamekusanyika London na kusema kuwa amefahamu kuwa muungano wa kujihami wa NATO hauna nia ya kuikubali Ukraine kujiunga nao, huku akiendelea kutoa mwito kwa muungano huo wa kutaka anga yake kufungwa. Zelenskiy aliyasema haya huku Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akiutahadharisha muungano wa NATO dhidi ya kukabiliana moja kwa moja kijeshi na Urusi.

Maryna alihojiwa kwa saa 14 na hakulala kwa siku 2

Huku hayo yakijiri, Ufaransa kupitia waziri wake wa mambo ya njeJean-Yves Le Drian, imetaka kulindwa kwa waandishi wa habari wanaoripoti kuhusu mzozo huo nchini Ukraine. kauli hii ya Le drian imekuja wakati ambapo mwandishi wa televisheni ya serikali ya kitaifa ya Urusi aliyekuwa amekamatwa baada ya kukatisha kipindi cha habari katika televisheni moja nchini humo kwa kupinga vita vinavyoendelea Ukraine, kutozwa faini na kuachiliwa huru.

Wagonjwa wa Ukraine wakimbilia Poland

01:39

This browser does not support the video element.

Mwandishi huyo Maryna Ovsyannikova ambaye anafanya kazi katika televisheni ya Channel 1, anasema alihojiwa kwa saa 14 na hakukubaliwa kulala kwa siku 2. Maryna aliingia studio hapo Jumatatu akiwa amebeba bango lililokuwa na maandishi "sitisha vita, musiamini propaganda, wanawadanganya hapa."

Vyanzo: Reuters/ https://www.dw.com/en/ukraines-zelenskyy-russian-demands-becoming-more-realistic-live-updates/a-61140204

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW