Zelenskiy asema hotosaini makubaliano ya kurefusha vita
1 Januari 2026
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema nchi yake inataka vita viishe, lakini si kwa gharama yoyote. Katika hotuba yake ya Mwaka Mpya, Zelenskiy alisema hatasaini makubaliano ya amani “dhaifu” ambayo yataendeleza vita.
Akiwa ofisini kwake, alisema Waukraine wamechoka baada ya karibu miaka minne ya vita, lakini hawako tayari kusalimu amri. Alisisitiza kuwa Ukraine inataka amani ya kudumu, si ya muda mfupi.
Zelenskiy alisema diplomasia inayoongozwa na Marekani, ikiwemo mazungumzo yake na Rais wa Marekani Donald Trump, imefanya makubaliano ya amani kuwa karibu kukamilika kwa asilimia 90. Hata hivyo, kikwazo kikubwa ni suala la nani atadhibiti maeneo ya ardhi ya Ukraine.
Urusi inadhibiti takribani asilimia 19 ya ardhi ya Ukraine, lakini Rais Vladmir Putin anataka Ukraine iondoe wanajeshi wake katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Donbas ambayo Moscow imeshindwa kuyakamata, madai ambayo Kyiv imeyakataa.