1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelenskiy: Ukraine yakabiliwa na hasara chungu Severodonetsk

15 Juni 2022

Vikosi vya Ukraine vinakabiliwa na hasara chungu katika mapigano na wanajeshi wa Urusi katika miji wa mashariki wa Severodonestsk na mkoa wa Kharkiv, amesema rais Volodymyr Zelenskiy siku ya Jumanne.

Ukraine | Zerstörte Häuser in Prywillja
Picha: Aris Messinis/AFP/Getty Images

Katika hotuba yake ya usiku wa manane rais Zelenskiy, alisema Ukraine inahitaji silaha za kisasa za kuzuwia makombora, na kuongeza kuwa hakuna sababu ya msingi kwa mataifa washirika kuchelewesha uwasilishaji wa silaha hizo. Baadhi ya makombora ya Urusi yanakwepa mifumo ya ulinzi na kusababisha vifo, alisema.

Ukraine imesema vikosi vyake vinajaribu bado kuwaondoa raia kutoka Severodonetsk baada ya Urusi kuharibu daraja la mwisho kuingia mjini humo.

Urusi imesema Jumatano kuwa imefungua njia ya kiutu kutoka kiwanda cha kemikali ya ammonia kilichoasisiwa chini ya utawala wa kiongozi wa Kisovieti Josef Stalin, kwenda mjini unaodhibitiwa na wanaotaka kujitenga.

Soma pia: Mashambulizi yaharibu daraja jingine Severodonetsk

Afisa wa juu nchini Ukraine amesema mapigano mjini Severodonestsk na maeneo mengine mashariki mwa nchi hiyo yanazidi kuwa magumu, lakini ameongeza kuwa wanajeshi wake wamemzuwia adui kwenye pande nyingine tatu kwa wakati mmoja.

Zelenskiy ameyataka mataifa ya magharibi kuipatia Ukraine mifumo ya kisasa zaidi ya kuzuwia makombora.Picha: Liselotte Sabroe/Ritzau Scanpix/AP/dpa/picture alliance

Gavana wa Luhansk Serhii Haidai amesema kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram, kwamba vita hiyo imezidi kuwa ngumu kwa jeshi la Ukraine, lakini akaongeza kuwa vikosi vyake vinaendelea kuilinda Severodonetsk na haviruhusu kusonga mbele kuelekea Lysychansk.

Kulingana na Haidai, pia kuna watu wengi waliojeruhiwa mjini Lysychansk, ulioko kwenye mto kutoka Severodonetsk.

Vikosi vya Urusi vinajaribu kupunguza kabisa upinzani wa Ukraine katika mji huo wa mashariki, katika juhudi pana za kuviondoa vikosi vya serikali kutoka mikoa miwili ya wanaotaka kujitenga ambayo Urusi inaiunga mkono na imeitambua kama mataifa huru.

Soma pia: Ukraine yasema idadi ya raia waliouawa imepindukia 12,000

Vita vya Severodonetsk, ambao ni mji wa takribani wakazi 100,000 kabla ya vita, hivi sasa ndiyo kitovu cha mapingano makali zaidi nchini Ukraine, wakati ambapo mzozo huo umebadilika na kuwa vita vya kudhoofishana.

Miito ya silaha za kisasa zaidi

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema baadhi ya maroketi ya Urusi yanakwepa mifumo ya ulinzi na kusababisha maafa makubwa.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy.Picha: Janis Laizans/REUTERS

''Leo mifumo yetu ya ulinzi wa anga imeweza kukata mbawa ya makombora ya Urusi. Tulifanikiwa kuangusha idadi ya makombora yaliyoelekezwa na wakaliaji kwenye miji yetu. Hii inamaanisha - maisha yaliyookolewa, vifaa vilivyohifadhiwa," alisema Zelenskiy.

Soma pia: Zelenskiy ataka Urusi itimuliwe FAO

"Lakini ni sehemu tu ya makombora tuliyoweza kuangusha. Kwa bahati mbaya tuna majeruhi na uharibifu. Leo, mikoa ya Lviv na Ternopil ilipigwa." "Na tunarudia kwa washirika wetu tena kwamba Ukraine inahitaji silaha za kisasa za kuzuia makombora."

"Nchi yetu haina silaha hizo kwa kiwango cha kutosha lakini ni sasa na katika nchi yetu ambapo mahitaji ya aina hii ya silaha ni makubwa. Ucheleweshaji wa kutoa silaha hizi hauna kisingizio.''

Wakati Rais Zelenskiy akiyasihi mataifa ya magharibi kuharakisha utoaji wa silaha kwa nchi yake, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema leo kuwa vikosi vyake vimeharibu ghala la silaha zilizotolewa kwa Ukraine na jumuiya ya NATO, karibu na mji wa Zolochiv katika mkoa wa Lviv.

Afisa wa utawala uliojitangazia jamhuri mkoani Luhansk Rodion Miroshnik, amesema karibu raia 1000 hadi 1200 wa Severodonetsk wanaweza kuwa bado kwenye eneo la kiwanda cha kemikali cha Azot, kwenye sehemu inayodhibitiwa bado na wanajeshi wa Ukraine.

Chanzo: Mashirika