1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelenskiy: Wiki hii ni muhimu kwa vita vya Ukraine

11 Aprili 2022

Taarifa za kijasusi za Uingereza zinasema majeshi ya Ukraine yamezuia mashambulizi kadhaa ya Urusi mashariki mwa nchi hiyo ambalo ndilo eneo linalolengwa mno na majeshi hayo kwa sasa.

Ursula von der Leyen trifft Präsident  Zelenskyj
Picha: Janis Laizans/REUTERS

Haya yanafanyika wakati ambapo Rais wa Ukraine Volodomyr Zelenskiy akisema wiki hii itakuwa muhimu mno kwa mkondo utakaochukua vita hivyo.

Majeshi ya Urusi yameachana na jaribio lao la kuuteka mji mkuu, Kyiev, na sasa juhudi zao zote sasa wanazielekeza mashariki mwa Ukraine. Taarifa za mara kwa mara za kijasusi zinazotolewa na Uingereza zinaeleza kuwa kumekuwa na mashambulizi ya mabomu katika maeneo ya Donetsk na Luhansk.

Taarifa hizo pia zinasema kuwa hatua ya Urusi ya kurusha mabomukiholela holela inaongeza hatari ya kuuwawa kwa raia. Mapema Jumatatu, kumeshuhudiwa miripuko mikubwa katika miji ya kusini na mashariki na ving'ora vimesikika kote nchini humo.

Mafuta ya Urusi yasinunuliwe

Serikali ya Ukraine kwa upande wake inasema imeandaa njia tisa za raia kuyakimbia mapigano mashariki mwa nchi hiyo.

Rais Zelenskiy (kulia) alipokutana na Waziri mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: Ukrainian Presidential Press Service/REUTERS

Majeshi ya Urusi pia yanafanya juhudi za kuuteka mji wa kusini wa Mariupol ambao ni mji muhimu sana na iwapo watauteka basi utakuwa unaunganisha magharibi na mashariki na miji ambayo tayari iko chini ya himaya yao.

Wakati hayo yakifanyika Rais Volodomyr Zelenskiy ameendelea na kampeni yake ya kutafuta uungwaji mkono wa kimataifa.

"Wanastahili kufanya kila wawezalo kuishurutisha Urusi itafute amani, wafanye kila wawezalo kuwachukulia hatua majeshi na makamanda wa Urusi kwa uhalifu wanaowafanyia watu wa Ukraine. Benki zote za Urusi ni lazima ziwekewe vikwazo, mafuta ya Urusi yasinunuliwe, uwezo wa Urusi kufanya uhalifu wa kivita ni sharti udhibitiwe," alisema Zelenskiy.

Zelenskiy ametoa wito huu wakati ambapo Kansela wa Austria Karl Nehammer anapanga kukutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi Jumatatu mjini Moscow na atatoa wito wa usitishwaji wa mapigano. Huu utakuwa mkutano wa kwanza kabisa wa Putin na kiongozi kutoka nchi za Ulaya tangu nchi yake ilipoanza kuivamia Ukraine Februari 24.

Maelfu ya watu wamefariki kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine

Viongozi hao wawili watakutana wakati ambapo wizara ya ulinzi ya Urusi inasema makombora yenye shabaha ya hali ya juu yameiharibu makao makuu ya kambi ya jeshi la Ukraine huko Dnipro katika mji wa Zvonetsky. Shirika la habari la Reuters limeripoti ingawa halikuweza kuthibitisha taarifa hizo.

Uvamizi wa Urusi umesababisha mauaji ya maelfu ya watu na uharibifu usiokadirika jambo lililopelekea mataifa ya Magharibi kuilaani Urusi na kuzua hofu kuhusiana na malengo ya Rais Putin.

Ludmila Zabaluk ni mkuu wa idara ya kijiji cha Dmytriv kaskazini mwa Kyiev na amesema katika hilo eneo lake, kumepatikana makumi ya miili ya raia ingawa shirika la Reuters halikuweza kuthibitisha ripoti hizo.

Chanzo: Reuters/DPAE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW